Wafanyakazi G4S mbaroni kwa wizi

CHRISTINA GAULUHANGA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa wanne wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya G4S kwa tuhuma za wizi wa Sh 1,280,000,000, Dola za Marekani 402,000 na Euro 27,700 mali ya Benki ya NBC walizokuwa wakizipeleka katika benki hiyo.

Pia inawashikilia askari wake nane wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa jeshi hilo kwa kukiuka maadili ya kazi wakati wa ufuatiliaji na upekuzi wa tukio hilo.

Akizungumza na wandishi wa habari leo Jumanne Februari 25, Kamanda wa Polisi, Razaro Mambosasa amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Februari 7, wakiwa na gari yenye namba za usajili T 728 BAN, aina ya Nisan Hard Body mali ya kampuni ya G4S.

Watuhumiwa hao ni Christopher Rugemalira (33), ambaye alikuwa dereva, Mohamed Athumani (40), Ibrahim Maunga (49) na Salum Shamte (45).

Imedaiwa badala ya kuzipeleka benki fedha hizo walipeleka gari hilo moja kwa moja Wilaya ya Temeke, Chang’ombe na kugawana fedha hizo kisha kutupa silaha chini.

Watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa na baadhi ya fedha huku nyingine wakiwa wamenunua magari zaidi ya mawili, nyumba zaidi ya moja na viwanja.