27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Wafanyakazi fichueni vitendo vya ukatili’

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAFANYAKAZI wameshauriwa kufichua vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi ili waweze kupata msaada wa kisheria.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Anna Kulaya.

Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa siku mbili baina ya shirika hilo na viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi.

Alisema sehemu ya kazi inapaswa kuwa salama kwa mfanyakazi kwani ni sehemu ambayo mfanyakazi anachukua muda mrefu kuishi.

“Kuna ukatili mkubwa sehemu za kazi na kwa kuwa nyinyi ni viongozi sehemu zenu za kazi mtakuwa mnajua zaidi kuliko sisi na tumewaita hapa siyo kutafuta mchawi bali kutafuta namna ya kutokomeza hali hiyo,” alisema Kulaya.

Alisema mwaka jana alituma timu ya wafanyakazi wake kwenda kuzungumza na wafanyakazi sehemu mbalimbali za kazi na walichokuta huko kinasikitisha sana.

Aidha, alisema wafanyakazi kwenye sehemu mbalimbali walizungumza kwa uwazi kuhusu rushwa ya ngono sehemu za kazi na ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa hasa wanawake.

“Tulichoona huko ndicho kimetusukuma kuandaa mdahalo wa leo baina yetu ili tujadiliane na tuangalie namna ya kuweka mifumo ambayo itakuwa na msaada mkubwa wa kukabiliana na hali hii,” alisema Mkurugenzi

Mwajina Lipinga kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi alisema serikali iliamua kuanzisha Mpango wa Kutokomeza Ukatili wa Wanawake na Watoto MTAKUWWA baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya.

Alisema wakati wa mchakato wa kuanzisha mpango huo wadau mbalimbali wakiwemo WiLDAF ambao alisema wamekuwa bega kwa bega na serikali katika utekelezaji wa mpango huo ambao unatarajiwa kufikia lengo mwaka 2022.

“Serikali iliona kuna shida kubwa kwenye ukatili hasa wanawake na watoto na lengo la MTAKUWWA ni kutokomeza  ukati kwa wanawake na watoto kwa asilimia 50 ikiwezekana kutokomeza kabisa,” alisema

Alisema maeneo ya umma na ya kazi si salama sana kutokana na vitendo vya ukatili vinavyofanyika hivyo wadau hao wananafasi kubwa ya kuzuia na kumaliza vitendo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles