Wafanyabishara wakamatwa kwa kuuza sukari bei juu

0
797

 EDITHA KARLO

SERIKALI mkoani Kigoma imeamuru kukamatwa na kuchukuliwa kwa leseni zao za biashara kwa wafanyabiashara watano wa mjini Kigoma ambao walikamatwa wakiuza sukari kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya Sh 3200 iliyowekwa na serikali.

Hatua hiyo imekuja kutokana na ziara ya ukaguzi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya Kigoma na viongozi wa wilaya hiyo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Samson Anga ambapo walifanikiwa kuwakamata wafanyabiashara watano wilayani humo wakiuza sukari kwa kukiuka bei elekezi ya serikali ya sukari ya Sh 3200 baada kukutwa wakiuza kilo moja ya sukari kwa Sh 3700.

Mkuu huyo wa wilaya aliamuru kukamatwa na kuhojiwa kwa watu hao kuhusiana na hali hiyo, kufunga maduka yao na kuchukua leseni zao za biashara hadi hapo hatua za kisheria dhidi yao zitakapomalizika.Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa wilaya alitembelea Soko Kuu la mjini Kigoma, Soko la Nazareth ambako alifunga maduka matatu na eneo la Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mkoani Masanga na kuamuru kuchukuliwa kwa leseni za wafanyabiashara hao wakisubiri utekelezaji wa hatua za kisheria dhidi ya makosa yanayowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ziara hiyo ya kushtukiza ni sehemu ya mpango mkakati wa kusimamia utekelezaji wa maelekezo na maagizo ya serikali kuona yanafuatwa na kutekelezwa na wafanyabiashara hao na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wale wote watakaotiwa hatiani.

“Serikali imejiridhisha kwamba hakuna uhaba wa sukari nchini na hakuna sababu ya bei ya bidhaa hiyo kupanda kwa kiwango hicho na wafanyabiashara wote wanatakiwa kufuata bei elekezi iliyotolewa na serikali na si kuwaumiza wananchi,” alisema DC Anga

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here