Na MWANDISHI WETU
Wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa nchini wametakiwa kushiriki katika shindano la utoaji tuzo bora kwa makampuni ya uzalishaji na watoa huduma itakayofanyika Machi, mwaka 2021 nchini Msumbiji katika mkutano wa mwaka unaoshughulikia vikwazo katika biashara kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADCTBT-Cooperation Structures).
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, Afisa Viwango Mkuu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Nickonia Mwabuka amesema tuzo hizo zinalenga kuangalia bidhaa za Tanzania zinazokidhi ubora katika utengenezaji na utumiaji kwa ajili ya wananchi na biashara pamoja na kukuza uchumi wa SADC.
“Tunawaomba wadau wote katika nyanja ya uzalishaji nna watoa huduma kutumia nafasi hii ya kushindana iliyotolewa na SADC, kujaza fomu husika kwa kuangalia vigezo vilivyowekwa na kutuma TBS kwa mtandao uliowekwa, kwa wale walioko karibu na ofisi zetu wanaweza kutuletea moja kwa moja mwisho wa upokeaji itakuwa siku ya Jumatano saa 10 jioni,” amesema Mwabuka.
Aidha, Mwabuka amesema makundi yote yatakayo shiriki watajaza fomu maalumu iliyoandaliwa ambayo ipo kwenye tovuti ya TBS- www.tbs.go.tz, ZBS- www.zbs.go.tz na kuirejesha kwa kutumia barua pepe ya [email protected] ambapo mwisho ni Novemba 25, mwaka huu.
Pamoja na hayo, Mwabuka amesema mshindi wa kwanza katika kila kundi atapewa cheti cha ushindani na kombe.
“Washindi hao pia watashiriki katika mkutano wa SADCTBT utakaofanyika Machi, 2021 Maputo nchini Msumbiji ambaye ndiye atakuwa Mwenyekiti wa SADC,” amesema Mwabuka.
Amesema kuwa faida ya kushiriki katika mashindano hayo ni pamoja na kufanya bidhaa na huduma za Tanzania kwa ujumla kujulikana katika soko la SADC.
Aidha, amesema sambamba na hayo makundi ambayo yatashiriki ambayo ni kundi la wajasiriamali chini ya watu 100, wazalishaji wakati na wakubwa zaidi ya wafanyakazi 100, mtu binafsi anayezalisha na kutoa huduma inayokidhi ubora.
“Utoaji wa tuzo kwa makampuni ya uzalishaji na watoa huduma ni utaratibu ambao hufanyika kila mwaka kwa wanachama wa SADC kwa lengo la kutambua mchango wa matumizi ya viwango katika kukidhi ubora wa bidhaa na huduma kwa jamii ya SADC,” amesema Mwabuka.
Tuzo ya hizo zimeandaliwa na Shirika la Viwango Tamzania (TBS) na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) wakishirikiana na Taasisi za sekta binafsi bara na visiwani.