TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Jiji la Dar es Salaam, Sporah Lyana, amewataka wafanyabiashara kujipanga kuanza kutoa huduma saa 24 katika stendi mpya ya mabasi inayojengwa Mbezi Luis na Kariakoo, akisema miundombinu ya CCTV kamera na mikakati ya ulinzi imeanza kuwekwa.
Sporah alisema hayo jana alipokuwa akizindua Wiki ya Huduma kwa Mteja, shughuli iliyoandaliwa na Benki ya NMB.
Akizungumza katika uzinduzi wa wiki hiyo, Sporah alisema maandalizi ya miundombinu ya kufanya biashara kwa saa 24 imeanza kuwekwa.
Alisema katika Soko la Kariakoo wameanza kufunga CCTV na taa za kutosha kuhakikisha biashara inafanyika kwa saa 24.
“Kwa sasa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (Lazaro Mambosasa) anajipanga katika masuala ya ulinzi kuwawezesha kufanya kazi kwa saa 24 kwa siku bila hofu ya uhalifu,” alisema Sporah.
Alisema katika Kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis kutakuwa na vyumba maalumu kwa taasisi za fedha, hivyo wanatakiwa kuomba nafasi hizo.
“Kituo hicho kitakuwa na maduka makubwa (shopping malls), hoteli na hosteli, na kitakuwa kikihudumia zaidi ya magari 1,000 kwa siku, hivyo ni fursa kwenu kutoa huduma zenu,” alisema Sporah.
Aliomba NMB kuendelea kutoa huduma bora kama ambavyo wamekuwa wakitoa na ikibidi kuziboresha zaidi.
“Niwapongeze NMB kwa kuwa mmekuwa mkichangia katika huduma mbalimbali za kijamii, ikiwamo sekta ya afya, elimu na huduma nyingine za jamii,” alisema Sporah.
Mkurugenzi wa Fedha wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuanzia sasa wameongeza muda wa kazi kwa matawi yake ya Mlimani City, Kituo cha Biashara cha Kahama na Kariakoo ambayo sasa yatafungwa saa moja jioni.
Alisema benki hiyo imeongeza matawi maeneo ya Mbogo mkoani Geita, Busega na Mbezi Luis na kufikia 230 yaliyopo kila wilaya na mawakala 6,000.
“Maboresho haya ni endelevu na kila siku tunajitahidi kuona tunaleta suluhisho kwa changamoto walizonazo wateja wetu katika sekta ya fedha,” alisema Ruth.
Alisema benki hiyi ilipokuwa inabinafsishwa mwaka 2005 ilikuwa na wateja 6,000, lakini sasa ina wateja zaidi ya milioni 3.5.
“Tuna mashine za fedha (ATM) zaidi ya 800 zinazopokea kadi za visa na master card,” alisema Ruth.
Alisema kutokana na huduma wanazotoa, wamepokea tuzo mbalimbali kitaifa na kimataifa kutambua ubora wao.
“Kwa miaka saba sasa jarida la Euromoney limeitambua NMB kuwa ni benki bora zaidi duniani,” alisema Ruth.