VERONICA KAZIMOTO-IFAKARA
WAFANYABIASHARA wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wameelimishwa kuhusu kodi ya zuio katika eneo la ukodishaji majengo na ardhi ambapo mpangaji anapaswa kukata kodi asilimia kumi ya kiasi cha malipo walichokubaliana katika mkataba wa upangishaji na kuwasilisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akizungumza wakati wa Kampeni ya Usajili, Huduma na Elimu kwa Mlipakodi inayofanyika mkoani Morogoro, Ofisa Kodi Mkuu, Julius Mjenga aliwataka wapangishaji kutowazuia wapangaji kukata asilimia kumi ya malipo ya mkataba kwa kuwa kodi hiyo inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato na inasimamiwa na TRA.
“Kodi ya zuio inatozwa kwa mujibu wa sheria na anayeisimamia sheria hiyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo wapangishaji wote mnapaswa kutowazuia wateja wenu ambao ni wapangaji wa majengo na ardhi kuwasilisha asilimia kumi ya malipo kufuatana na mkataba mlioingia,” alisisitiza Mjenga.
Alisema kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wapangishaji kuwakatalia wapangaji wao kukata asilimia hiyo na pale wanapolazimisha husitishiwa mkataba au kupewa notisi ya siku 90.
“Iwapo mpangishaji atakaidi malipo hayo ya asilimia kumi yasikatwe na mpangaji kwa lengo la kuyawasilisha TRA, mpangishaji huyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015,” alisema Mjenga.
Kodi ya zuio inatozwa katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara, mirabaha, hisa, upangishaji na gawio mbalimbali ambapo kila eneo limepangiwa kiwango cha asilimia kinachotakiwa kulipwa.
Kampeni ya usajili, huduma na elimu kwa mlipakodi imeanza juzi na itamalizika Novemba 17, na itafanyika katika wilaya zote za mikoa ya Morogoro na Pwani.