22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WAFANYABIASHARA TUNDUMA WAHAMIA ZAMBIA

Na ELIUD NGONDO-SONGWE


MKUU wa Mkoa wa Songwe, Chiku Gallawa ametoa siku 14 kwa Mkuu wa Wilaya ya Momba, Juma Irando na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma  a na watendaji wa Mamlaka ya  Mapato Tanzania (TRA) kufanya uchunguzi wa haraka  kubaini  iwapo kuna wafanyabiashara waliohamishia biashara zao  Zambia.

Akizungumza jana katika mkutano na wafanyabiashara mjini Tunduma, Gallawa alisema ameagiza viongozi hao kufanya utafiti kwa haraka kubaini kama wafanyabiashara wa Tanzania wamehamishia biashara zao nchini humo.

Inadaiwa kuwa wafanyabiashara wamehamishia biashara zao Zambia kutokana na vikwazo kutoka TRA vikiwamo utitiri wa kodi tofauti na Zambia.

“Eneo la Tunduma ni dogo kiasi ambacho inatakiwa kuchunguzwa kutambua ni kwa nini wafanyabiashara hao wamehama kwenda kufanya biashara hizo   Zambia.

“Na imani ni kuwa uchunguzi ukishafanyika tutajua ni njia gani ya kuwarudisha na wakaendelea na shughuli zao,” alisema Gallawa.

Alisema   wafanyabiasha wa Tunduma walizoea kufanya biashara bila kulipa kodi  hivyo kuwapo mabadiliko ya sasa inawezekana ikawa ni chanzo cha wao kuhamia   Zambia na kuanzisha biashara zao huko.

Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Paul Alalaze alisema malalamiko ya wafanyabiasha yamekuwapo kwa muda mrefu yakiwamo ya viwango vya utozwaji wa kodi vikidaiwa kuwa vikubwa tofauti na Zambia.

Alisema kutokana na wafanyabiashara wengi wa Tanzania kuhamia Zambia zinafanyika jitihada za kuwaelimisha  waendelee kufanya shughuli zao  nchini mwao.

“Tunawaelimisha kuwa wanatakiwa warudi kufanyia shughuli zao Tanzania ili kuendelea kujenga uchumi wa nchi yao na si kukimbilia Zambia ambako si kwao kwa sababu  wananufaisha watu wengine,” alisema Alalaze.

Baadhi ya wafanyabiashara walisema  idadi ya wenzano wanaohamishia miradi yao   Zambia inazidi kuongezeka.

Wameitaka Serikali   kufanya uchunguzi   kubaini ukweli wa malalamiko hayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Harid Kain ambaye ni mfanyabiashara  Tunduma, alisema kitendo cha wafanyabiashara kuhamia nchi jirani ni changamoto ambayo inasababisha Tanzania kukosa mapato na wananchi wake wakibaki kukosa huduma za msingi.

“Zinatakiwa jitihada za makusudi kuhakikisha wafanyabiashara wote waliohamia Zambia wanarudi kuendelea na biashara zao kama ilivyokuwa awali na mapato yaendelee kukusanywa na Serikali ya Tanzania.

Mfanyabiashara mwingine, Ally Mapumba alisema maofisa biashara wanatakiwa kukaa na wafanyabiashara wa Tanzania kujadili na kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili na kuzitatua ili   biashara iendelee kama ilivyokuwa zamani.

“Kwa nini wafanyabiashara wa Tanzania wahamishie biashara zao   Zambia wakati mazingira ni haya haya?

“Hivyo ni jukumu la maofisa biashara wa Tanzania kukaa na wafanyabiashara kutafuta ufumbuzi wa  changamoto zote zinazolalamikiwa,” alisema Mapumba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles