BAADHI ya wafanyabiashara wa Mwanza wanaendelea kufanya biashara zao kwa kuuza bila ya kutoa Stakabadhi za Mashine za Elektroniki (EFD).
Wafanyabiashara hao wanadai wanangoja Serikali ianze kuwasambazia mashine hizo.
Kwa sababu hiyo wamekuwa wakitoa stakabadhi za kawaida hali ambayo inaelezwa kuwa huenda imekuwa ikiikosesha mapato Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotaja majina yao, walidai Serikali iliahidi kuzigawa mashine hizo bure kwa wafanyabiashara waweze kuzitumia kulipa kodi pale mteja anaponunua bidhaa zao lakini hadi sasa hazifikishwa.
Walisema baada ya ahadi ya Serikali kutolewa, mashine hizo zilitolewa kwa wafanyabiashara wa Dar es Salaam lakini mpaka sasa hawajui ni lini zitafikishwa na kusambazwa mkoani Mwanza.
Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuzigawa mashine hizo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Ernest Dundee, alisema suala hilo liko juu ya uwezo wake kwa sababu anayetakiwa kuelezea mashine hizo ni kamishna mkuu wa mamlaka hiyo.
“Ninachojua wapo baadhi ya wafanyabiashara wanazo mashine hizo za EFD na wanazitumia lakini wale ambao hawana wanatakiwa kutekeleza sheria za ulipwaji wa kodi na wanapaswa kutoa stakabadhi.
“Suala la mashine kusambazwa bure mimi siwezi kulizungumzia ni vema mkamuuliza kamishna mkuu kule Dar es Salaam.
“Lile ni tamko la taifa, sasa utekelezaji wa tamko hilo unaamuliwa huko huko, mimi hapa sina uamuzi wowote,” alisema.
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) ambao wamekuwa katika mgogoro w amuda mrefu na TRA juu ya matumizi ya stakabidhi ya EFD na kusababisha maduka kufungwa.
Wafanyabiashara hao chini ya Mwenyekiti wao wa JWT, mkoa wa Mwanza, Christopher Wambura wamekuwa na msimamo mkali juu ya suala hilo.
Kitendo cha kufungwa maduka husababisha TRA kushirikiana na polisi kuwaonya wale wanaohamasisha au kuwatisia wafanyabiashara walio na EFD kutotumia mashine hizo.