Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Kinondoni umewaonya baadhi ya wafanyabiashara wanaopunguza uzito wa bidhaa zinazofungashwa viwandani kuwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini na kufikishwa mahakamani.
Hatua hiyo inafuatia ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na wakala huo katika maeneo mbalimbali yanayohifadhi bidhaa za vyakula na ujenzi ambao ulibaini sukari imepunguzwa uzito wa kati ya kilo moja hadi kilo moja na nusu.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo uliofanywa katika baadhi ya maghala yaliyopo Kigogo mwisho Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kinondoni, Charles Mavunde, amesema wamewakamata wafanyabiashara wawili na kuwafikisha polisi ambapo baada ya kukiri kosa walitozwa faini.
“Tuko kwenye zoezi la ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo mbalimbali yanayohifadhi bidhaa za vyakula na vifaa vya ujenzi ili kuona kama zina uzito sahihi.
“Tumekwenda katika ‘godown’ moja tulipopima sukari tulipata wastani wa kilo 24 badala ya kilo 25 zilizoandikwa kwenye kifungashio na kilo 48.5 kwa vifungashio vya kilo 50, sukari imepunguzwa karibu kilo moja na nusu. Bidhaa kabla haijatoka kiwandani huwa inakaguliwa kuangalia kama uzito uko sawa lakini wakati mwingine inachezewa njiani ,”amesema Mavunde.
Mavunde amesema kulingana na Sheria ya Vipimo sura 340, mtu anayekiri kosa adhabu ni faini kati ya Sh 100,000 hadi Sh milioni 20 na iwapo atarudia kosa adhabu ni faini kati ya Sh 300,000 hadi Sh milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka mitano.
Kuhusu vifaa vya ujenzi amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia vifungashio visivyoandikwa maandishi yoyote na wakati mwingine kupunguza uzito.
“Mfano tumekamata misumari tulipoipima tukakuta ina uzito sawa lakini kile kifungashio hakijaandikwa chochote sasa mteja hatashindwa kujua imetengenezwa wapi na ubora wake ukoje,” amesema Mavunde.
Kaimu Meneja huyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kujitahidi kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha bidhaa zina uzito kama ilivyoandikwa kwenye vifungashio huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano pale wanapobaini bidhaa ina uzito pungufu.