Na Mwandishi wetu |
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, imetupilia mbali kesi ya wafanyabiashara wa Kigoma dhidi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji katika kesi ya kupinga sheria ndogo ya Manispaa hiyo kuhusu tozo la ushuru wa pango wa Sh 50,000 kwa mwezi iliyofunguliwa na wafanyabiashara hao.
Mahakama hiyo imewataka wafanyabiashara hao kuendelea kulipa kulipa tozo ya pango ya kiasi hicho cha fedha.
Hukumu hiyo imetolewa siku chache baada ya Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole kutoa tamko la kuwaruhusu wafanyabiashara hao wasilipe Sh 50,000 kama tozo ya pango katika vibanda vyao.
Akitoa uamuzi wa shauri hilo, Jaji wa mahakama hiyo aliyekuwa anasikiliza shauri hilo, Julius Mallaba amesema tozoa iliyopandishwa na Manispaa ilifuata taratibu zote na kusainiwa na Waziri mwenye dhamana na kutangazwa kwenye Gazeti la serikali.
Kesi hiyo namba moja ya mwaka 2018, ilifunguliwa Februari mwaka huu na mfanyabiashara Raymond Ndabhiyegetse, kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake dhidi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambao katika maombi yao waliitaka mahakama hiyo kupinga sheria ndogo na kupitia upya sheria hiyo.