29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Machinga Complex kujitangaza kimataifa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wafanyabiashara katika Soko la Machinga Complex wanatarajia kukuza masoko na ufanisi wa biashara zao baada ya kuwepo huduma ya intaneti watakayotumia bure.

Katibu wa Wafanyabiashara wenye ulemavu Mkoa wa Dar es Salaam, David Nyendo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya intaneti iliyofungwa katika Soko la Machinga.

Hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini na teknolojia ya 5G, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema Serikali itaweka Wi – Fi ya bure Machinga Complex, vituo vya mwendokasi na vyuo vikuu.

Akizungumza Agosti 13, 2023 na wafanyabiashara hao Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka kutumia intaneti hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili wafaidike kiuchumi.

“Huduma ya intaneti itawasaidia wafanyabiashara kutangaza biashara zao ili zifahamike na kuwawezesha wateja kufika kwa urahisi bila kupotea,” amesema Mpogolo.

Katibu wa Wafanyabiashara wenye ulemavu Mkoa wa Dar es Salaam, David Nyendo, amesema wanapata faraja kwa jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali za kuboresha mazingira ya kufanyia biashara.

“Mbali na hii intaneti Serikali imetufanyia mengi tangu mheshimiwa Rais aingie madarakani, kuna vyuo vya watu wenye ulemavu ambavyo vilijengwa zamani na Mwalimu Nyerere lakini vilikuwa vimefungwa, amevifungua vyote na wanafunzi wenye ulemavu wanasoma bure,” amesema Nyendo.

Meneja wa Machinga Complex, Stella Mgumia, amesema kufungwa kwa mtandao huo kutasaidia kuwatangaza wafanyabiashara na kuwataka ambao hawana maeneo rasmi kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa ikiwemo Machinga kwa kuwa kuna nafasi za kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles