Mwandishi Wetu, Kagera
Serikali imetangaza mkakati wa kuanza kugawa mabehewa kwa wafanyabiashara ili waweze kusafirisha mizigo yao kwa usafiri wa treni na meli kama njia ya kuimarisha sekta ya uchukuzi kupitia usafiri huo.
Mabehewa hayo zaidi ya 1,000 yanayomilikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa wafanyabiashara wakubwa ambao watahitaji kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kutoka bandarini kwenda mikoani.
Akizungumza leo katika Bandari ya Bukoba na baadaye Kemondo Bay zilizopo mkoani Kagera, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema mchakato huo wa kutoa mabehewa hayo utaanza baada ya kufanyika kikao kati yake na wadau mbalimbali wakiwamo wafanyabishara wanaotumia usafiri wa meli na reli kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao.
“Mabehewa hayo watakayopewa wafanyabishara hao wanaohitaji pamoja na kuyafanyia matengenezo kwa fedha zao bado yatabaki kuwa mali ya TRC.
“Mabehewa ambayo tunayo pale TRC tutawapa wafanyabiashara na sisi tutawaruhusu kutumia miundombinu ya reli lakini tutakuwa tukipata ushuru unaotokana na kutumia reli.
“Hivyo kati ya siku mbili hizi nitakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Kadogosa ili kujadili kwa kina suala hilo ambalo sasa litatufanya turahisishe utoaji wa huduma za usafiri, tunaka tukimbie badala ya kuendelea kwani imetuchelewesha sana,” amesema Kamwelwe.