24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 23, 2023

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Dodoma wamwangukia Lukuvi

Lukuvi+PHOTONA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WAFANYABIASHARA wa Soko la Sabasaba mkoani Dodoma wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuwafuta kazi watendaji wa Serikali ambao wameuza nyumba za Serikali kinyume cha sheria.

Wakizungumza na MTANZANIA jana mjini hapa, walisema wamekuwa wakifanya biashara katika soko hilo kwa muda mrefu, lakini hivi sasa wanashangaa kuelezwa kuwa wanatakiwa kuhama kwani jengo hilo limeuzwa kwa mtu binafsi.

Walidai jengo hilo lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Afya kwa muda mrefu, lakini wanashangazwa na hatua ya Serikali kuliuza kwa mtu binafsi badala ya kutoa nafasi kwa wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara zao.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Huseni Michuzi,  alisema  kwa muda mrefu wapo katika eneo hilo, lakini wanashangaa Serikali kuwataka kuhama wakidai eneo hilo si halali kwao.

“Hili ni soko, hapa tunafukuzwa tupo zaidi ya watu 15, tunaambiwa hili eneo kauziwa mtu binafsi, sasa tunajiuliza mtu binafsi anaweza kuuziwa mali ya Serikali? Tunamwomba Waziri Lukuvi awafute kazi wote waliohusika na dili hili kwani wametumia madaraka yao vibaya,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo, Athumani Makole, alisema alipokea malalamiko ya wafanyabiashara 15 wakitakiwa kuhama katika eneo hilo ambalo linadaiwa ni mali halali ya Solomoni Munuo.

“Lile eneo lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya maonyesho ya Nanenane, baadae ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilitupa maelekezo kuwa ni eneo la walemavu sasa tunashangaa Munuo kudai ni eneo lake,’’ alisema.

Kwa upande wa aliyeuziwa jengo hilo, Munuo, alisema eneo hilo ni mali yake aliyokabidhiwa kihalali na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kushirikiana na manispaa baada ya kuona jengo hilo halitumiki.

Akifafanuzi kuhusu suala hilo, Ofisa Masoko wa Manispaa ya Dodoma, Steven Maufi, alisema kutokana na vielelezo vilivyo  eneo hilo ni mali ya Munuo hivyo ana haki ya kuwaondoa watu waliokuwa mbele ya nyumba yake.

“Hilo ni eneo halali la Munuo ndiyo maana tukaamua kuwaondoa wafanyabiashara walio mbele yake, lakini pia wamekuwa wakisababisha uchafu kutokana na kumwaga chini takataka,’’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,093FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles