26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara 10 Kariakoo mikononi mwa Takukuru

Na EVANS MAGEGE

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imenasa wafanyabiashara wakubwa 10 wa maduka katika eneo la Kariakoo kwa tuhuma za udanganyifu wa kulipa kodi kwa serikali.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo  alisema wafanyabiashara hao wamekamatwa ndani ya wiki mbili tangu kuanza kwa operesheni ya kuwasaka wafanyabiashara wanaofanya udanganyifu wa kulipa kodi katika biashara zao jijini Dar es Salaam.

Brigedia Jenerali Mbungo aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Masai  Shop , Malya Shop, Noa Tiles, Kanda Trading Company, Chengula Investment Company.

Wengine ni Tamara Traders Company, Mchapakazi  Home Appliance, Kisangani General Enterprises  Ltd, Kipata Cafeteria na Kiwanso Builders Corner.

Alisema wafanyabiasha hao wote wamepatikana katika operesheni  inayoendelea katika eneo la Kariakoo.

Alisema Takukuru ni chombo chenye dhamana ya kusimamia  mapambano dhidi ya rushwa nchini na inaongozwa na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11 ya 2007.

Alisema sheria hiyo inatamka makosa 24 ya rushwa yakiwamo kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya muajiri au kupitisha fedha kwa ufisadi kinyume na kifungu cha 22 cha sheria hiyo.

Alisema kutokana na kifungu hicho adhabu ya kutenda kosa ni faini isiyozidi sh milioni saba au kifungo cha miaka mitano jela au adhabu zote kwa pamoja.

Pia alisema sheria hiyo katika kifungu cha 32  kinakataza kula njama kwa lengo la kula  rushwa ambapo adhabu yake ni faini ya sh milioni tano au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

“ Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kutokukusanya kodi ni sifa moja ya nchi iliyogubikwa na rushwa,  sasa kama tunavyofahamu kodi ndio chanzo cha mapato kwa taifa lolote pia ndiyo inayotumika kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya taifa,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

MBINU WANAYOTUMIA KUKWEPA KODI

Brigedia Jenerali Mbungo alitaja sababu 10  ambazo taasisi yake imezibaini kutumiwa na wafanyabiashara hao kukwepa kulipa kodi.

Sababu hizo ni wafanyabiashara kutoza risiti zenye kiasi tofauti na kiasi cha pesa halisi kilichotolewa ili kununua bidhaa husika.

Wafanyabiashara kuwaambia wateja kuwa wanawapa risiti ya kutembelea tu ili waioneshe endapo watakutana na maafisa wa TRA na kuwauliza kuhusu risiti ya mzigo au bidhaa waliyonunua.

Baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti za kielektroniki baada ya kufanya mauzo.

Sababu nyingine ni kujichelewesha kutoa risiti kwa lengo la kumtegea mteja kama atadai au hatadai risiti.

Baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti hata baada ya mteja kuomba kupatiwa risiti humweleza kuwa bidhaa alizonunua ni chache.

Pia wafanyabiashara wengine wamekuwa wakiwapatia wateja risiti za kughushi na baadhi wanawapatia wateja risiti za kughushi ambazo ni za bidhaa tofauti  na bidhaa iliyonunuliwa.

Alitaja sababu nyingine walizobaini  ni wafanyabiashara kutotoa risiti na badala yake huwaandikia wateja orodha ya bidhaa kwenye karatasi na kuwaelekeza kuwa waende wakachukue mzigo kwenye stoo zao.

Kwamba katika mazingira hayo mteja akishachukua mzigo na asiporudi tena dukani ni wazi kuwa hatapewa risiti.

“ Wapo wafanyabiashara ambao wanawapatia machinga bidhaa zao ili wasilipe kabisa kodi na kwa upande mwingine wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakifurahia kupewa punguzo la bei kwa sharti la kutopewa risiti,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles