25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wafamasia waonywa uuzaji dawa kiholela

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

RAIS wa Baraza la Famasia Tanzania, Issa Hango amewatahadharisha wafamasia wanaouza dawa bila kufuata maadili, kwani hali hiyo inaweza kusababisha madhara ya usugu wa vimelea unaosababishwa na matumizi holela ya dawa za antibiotiki (vijiuasumu).

Alisema ni kosa la kisheria kwa mfamasia kuuza dawa kwa mgonjwa bila ya kuona cheti cha daktari kwani hatua hiyo inaweza kuathiri afya ya binadamu au hata mnyama.

Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, Hango alisema kuwa ni vyema hata jamii ikafuata maagizo wanayopewa na wataalamu katika matumizi ya dawa.

“Madhara ya matumizi ya dawa kiholela ikiwamo dawa bandia na zile ambazo muda wake umeisha, ni hatari kwa afya kwani husababisha usugu wa vimelea.

“Tunajaribu kuangalia kuna dawa watu wanapata bila kuwa na cheti cha daktari,  huu ni ukiukwaji wa maadili, na watu kama hawa tunawachukulia hatua za kinidhamu.

“Kitu cha kwanza wauzaji wanatakiwa kuelewa na kufuata maadili ya maelekezo ya matumizi ya dawa na uuzaji wa dawa hizo, kwani kuna wale wafamasia ambao wanauza dawa kiholela bila kujali mtu anayempatia anaweza kuathirika.

“Wauzaji wa maduka ya dawa waache tamaa ya fedha, badala yake watangulize utu mbele, hii itasaidia kuokoa afya za watu kwani madawa yanaweza kuponya au kuangamiza,” alisema Hango.

Alisema kuwa kutokana na matumizi holela ya dawa, madhara ni makubwa, kwamba watu 70,000 duniani kote wanapoteza maisha kutokana na usugu wa vimelea vinavyosababishwa na matumizi ya antibiotiki, hivyo umakini pia unahitajika kwa jamii.

“Lakini bado tunahitaji msaada wa jamii katika kutoa taarifa na kutokwenda kuchukua dawa famasi bila kupitia kwa daktari, kwani mtu unavyofanya hivyo unahatarisha afya yako mwenyewe.

“Hivyo mtu akiumwa ni bora akaenda kumwona daktri ili kuandikiwa dawa inayokufaa, hii itakusaidia kuepukana na usugu wa vimelea,” alisema Hango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles