24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Wafa katika msongamano kampeni za Buhari

LAGOS, NIGERIA


WATU kadhaa wameripotiwa kufariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya umati wa watu waliofurika katika mkutano wa kampeni za Rais Muhammadu Buhari anayetetea kiti chake kukanyagana.


Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza – BBC, tukio hilo lilitokea jana katika uwanja wa mpira wa Adokiye Amiesimaka uliopo kusini mwa mji wa Port Harcourt, baada ya umati huo wa watu kusongamana na wengine kuanguka na kukanyagwa katika lango kuu baada ya hotuba ya Rais Buhari kumalizika.


Taarifa nyingine zinaeleza kuwa wengi wa waathiriwa wameripotiwa kuanguka na kukanyagwa na wenzao waliokuwa wakijaribu kuingia uwanjani kupitia lango lililokuwa limefungwa ili kumfuata Rais Buhari aliyekuwa ameondoka katika uwanja huo.


Watu walioumia walipelekwa katika hospitali iliyo karibu kupata matibabu.
Ofisi ya rais ilisema kuwa Rais Buhari aliarifiwa kuhusu tukio hilo na akaelezea kusikitishwa kwake.


“Tunasikitika kwamba wengi wa wliofariki ni wafuasi wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC),” ilieleza taarifa ya ofisi hiyo ingawa haikutaja idadi ya watu waliofariki dunia.


Lakini msemaji wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Port of Harcourt, Ken Daniel Elebiga alikaririwa na Shirika la habari la AFP akisema kuwa karibu miili ya watu 15 ilifikishwa hospitalini hapo.


“Kuna wengine wapo chini ya tahadhari ya matibabu katika Kitengo cha Dharura, hivyo hatuwezi kulazimisha takwimu wazi zaidi ya hali ilivyo wakati huu,” alisema Daniel-Elebiga.

Wanigeria watapiga kura Jumamosi kumchagua rais huku kinyang’anyiro kikali kikitarajiwa kuwa kati ya Rais Buhari na Makamu Rais wa zamani, Atiku Aboubakar.
Vyama 73 vimejiandikisha kugombea nafasi ya urais huku kukiwa na wapigakura milioni 84.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles