21.4 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wapendekeza viongozi wa dini wahusishwe ajenda ya wanawake, amani, usalama

 Na Norah Damian, Mtanzania Digital

Wadau mbalimbali wamependekeza viongozi wa dini wahusishwe katika Mpango kazi wa kitaifa juu ya ajenda ya wanawake, amani na usalama.

Ajenda hiyo ya Umoja wa Mataifa ilipitishwa mwaka 2000 na Tanzania ilianza mchakato wa kutengeneza mpango kazi huo mwaka 2019 ambapo Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutetea Haki za Wanawake (UN WOMEN TANZANIA) ndio wanaratibu.

Mwanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, Munira Surve, akizungumza wakati wa mkutano wa kukusanya maoni kwa ajili ya Mpango kazi wa kitaifa juu ya ajenda ya wanawake, amani na usalama.

Wadau hao kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, wanazuoni, vikundi vya kinamama, wanafunzi na vijana wametoa mapendekezo hayo leo Desemba 21,2022 wakati wa mkutano uliokuwa na lengo la kukusanya maoni kwa ajili ya mpango huo.

Mmoja wa washiriki katika mkutano huo, Michael Gerorge, amesema viongozi wa dini wana umuhimu mkubwa katika mpango huo kwa sababu watasaidia kusukuma ajenda mbalimbali kwa manufaa ya taifa.

“Viongozi wa dini wakisema kitu wanaaminiwa hivyo wakijumuishwa katika mpango huu watasaidia sana kusukuma ajenda,” amesema.

Naye mwanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, Munira Surve, amependekeza kuanzishwa kwa klabu kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuhimiza masuala ya wanawake, amani na usalama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Umoja katika Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Profesa Ikaweba Bunting, amesema watahakikisha sera itakayotengenezwa juu ya masuala hayo inafanana na historia ya Tanzania.

“Sisi ni kisiwa cha amani, tunapokea wakimbizi na watu wamekuwa wakiuliza kitu gani kinafanya Tanzania iwe na amani hivyo, tukitengeneza sera ikaonyesha historia, mila na desturi za Tanzania kuna amani inaweza kusaidia nchi zingine za Afrika,” amesema Profesa Bunting.

Mratibu Msaidizi wa mpango huo ambaye pia ni Ofisa Programu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Eliud Kabamanya, amesema hatua ya sasa ni ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau ili yaingizwe katika mpango huo ambapo wanatarajia hadi kufikia Januari 30 mwakani watakuwa wamekamilisha na kukabidhi serikalini.

Amesema mikutano hiyo itafanyika Dar es Salaam na Zanzibar kwa kushirikisha makundi mbalimbali ya wadau na kwamba baada ya kupata maoni yataingizwa kwenye rasimu ya mwisho itakayokabidhiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuurasimisha mpango kazi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles