29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau waomba Serikali kuitazama upya sheria ya vyombo vya habari

*Wapendekeza magazeti kupewa Usajili wa kudumu

*Wasiolipa matangazo kwa wakati pia kudhibitiwa

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa toaji leseni za magazeti kutoka mfumo wa sasa wa kila mwaka badala yake yapewe usajili wa kudumu uliokuwa ukitumia awali.

Aidha, imeshauriwa kuwepo kwa sheria ya adhabu ya miezi sita jela kwa kampuni zitakazoshindwa kulipa fedha za matangazo kwa vyombo vya habari ndani ya siku 30.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Jukuwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile katika mkutano maalumu uliofanyika kwa njia ya mtandao ulioandaliwa na jukwaa kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini.

Balile alisema kuna mambo mengi yanayopaswa kutazamwa upya ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa kifungu kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), madaraka ya kuratibu matangazo yote ya serikali.

“Ili vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru lazima baadhi ya vifungu viondolewe katika sheria ya sasa, miongoni mwa hivyo ni pamoja na utaratibu wa kutoa leseni kwa magazeti unaotumika hivi sasa.

“Wote ni mashahidi kwamba tumeshuhudia ukitumika vibaya kufifisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Mfano tumeshuhudia kusitisha leseni za magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto, na kufuta Tanzania Daima, je utaratibu huu una faida yoyote zaidi ya kuua Uhuru wa Vyombo vya Habari?,”amehoji Balile.

Balile amesema kuwa kuna haja ya kurejea kwenye utaratibu wa awali ambapo gazeti lilikuwa linajiendesha bila kuwapo kwa utaratibu wa kufutwa baada ya kusajili.

“Je, kwa nini tusirudi katika utaratibu wa zamani ambapo gazeti lilikuwa linasajiliwa na kujiendesha bila kufutwa kama ilivyo sasa? mazingira yakiwa vizuri, sheria zikawa nzuri, matangazo yakatolewa kwa bei stahiki badala ya sasa ambapo wanashusha bei watakavyo, mapato ya vyombo vya habari yataongezeka,” amesema Balile.

Balile amesema kuwa idara ya Habari Maelezo inapewa madaraka na Sheria hii kifungu cha 5 (l) kuratibu matangazo yote ya Serikali na kwamba serikali haioni kuwa kifungu hicho kitapunguza ufanisi wa kutoa na kusambaza matangazo nchi nzima ikiwemo kuweka mazingira ya rushwa.

Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kumekuwa na malalamiko kwamba waandishi wa habari hawalipwi ipasavyo lakini ikiwa mapendekezo haya yatafanyiwa kazi, malipo yatapatikana kwa wakati na ubora wa habari utaongezeka nchini.

“Kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Juni 28, 021 kwamba vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani, tunapenda sana vyombo vya habari vipewe matangazo kwa njia ya ushindani na sio kwa njia ya upendeleo au kwa njia ambazo zinaleta mashaka kwa hiyo tutaendelea kuzungumza.

“Na tunamshukuru waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye amesema mara zote tutaendelea kuzungumza, tutaelewana mpaka vifungu vipi vifike hatua ipi kwa ajili ya kuwa na sheria iliyo bora kabisa inayoruhusu uhuru wa vyombo vya habari, lakini zinaweka wajibu kwa watendaji na waandishi kwa maana kwamba kila uhuru, kila haki inakuja na wajibu wake,” amesema Balile.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye.

Upande wake, Mwandishi wa Kituo Cha runinga cha ITV, Godfrey Monyo amesema kuwa pamoja na mambo yote hayo lakini suala la elimu kwa wanahabari lazima lizingatiwe.

“Elimu ni kitu muhimu kwa taaluma, ili kazi zifanyike vizuri lazima elimu izingatiwe ili tusionekane wanataaluma flani wakati huduma yetu inahitaji elimu,” amesema.

Akichangia mjadala huo, Wakili James Marenga amesema suala la elimu kwamba kila anayefanya kazi ya habari kuwa na ukomo wa elimu kama ilivyo kwa taaluma nyingine.

Amesema sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ikiwemo Sheria ya Kupata Taarifa ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 kuna baadhi ya vifungu au vipengele ambavyo vina changamoto ambavyo vikifanyiwa mabadiliko vitawezesha sheria hizo kuleta ufanisi.

“Kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kwa maendeleo ya nchi na ni jambo lisilohitaji msisitizo mkubwa sana kwa sababu umuhimu wake unajulikana.

“Hivyo, kutungwa kwa sheria rafiki kwa vyombo vya habari kutawawezesha wadau wote wa habari wakiwemo waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria kwa manufa ya serikali na umma,”amesema Marenga.

Wakili James Marenga.

Amesema, miongoni mwa vifungu ambavyo vina mapungufu katika sheria hiyo ni pamoja na 4 (1), 5 (1), 6(1),7(1), 7(3), 9, 11, 22(1) na 22(2) ambavyo vinazungukwa na neno “Intentionally” (kwa kudhamiria).

“Kuna umuhimu wa kurekebisha sheria na kufuta neno “kwa kudhamiria”. Haiwezekani kuthibitisha nia ya kufanya uhalifu kwa maneno ya kubahatisha,”amesema Marenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles