25.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wahamasishwa kuchangamkia fursa za uwekezaji Tabora

Na Allan Vicent, Tabora

Wadau wa Maendeleo kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora wameshauriwa kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika Mkoa huo ili kujiongezea mapato ikiwemo kuchochea maendeleo ya Mkoa huo.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Geofrey Mwambe alipokuwa akizindua ‘Mwongozo wa Fursa za Uwekezaji Mkoani Tabora’ katika hafla maalumu iliyofanyika jana mjini hapa.

Alisema Mwongozo huo ni muhimu sana kwani utawezesha wadau kujua vivutio na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizoko mkoani humo huku akipongeza uongozi wa Mkoa huo kwa jinsi ulivyojipanga vizuri kutoa ushirikiano kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kuja kuwekeza.Mkoani humo.

Aliwataka wadau wa maendeleo walioko ndani ya mkoa huo kuwa wa kwanza kuchangamkia fursa hiyo huku akishauri wajikite kwenye uwekezaji wenye tija na sio kuishia kwenye maneno tu kama baadhi ya Mikoa inavyofanya.

Alisisitiza kuwa uwekezaji ni kichocheo muhimu sana cha maendeleo ya Mkoa
husika na taifa kwa ujumla na hata Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imelipa kipaumbele kikubwa suala la uwekezaji.

“Naupongeza sana Uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa kuja na wazo lenye maslahi  mapana kwa jamii, Mkoa na Taifa kwa ujumla, kwa kuwa uwekezaji utaongeza fursa za ajira na kuinua uchumi wa wananchi,” alisema.

Waziri Mwambe alihimiza wakazi wa Mkoa huo na Mikoa jirani kutumia Jukwaa hilo kama fursa ya kuanza kulima mazao mbalimbali ikiwemo mbegu zitoazo mafuta kwa wingi ili kuzalisha mafuta mengi ya kula na yenye ubora kwa ajili ya viwanda na matumizi ya kawaida ili kuleta ushindani kimasoko.

Alimhakikishia Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Philemon Sengati na wakazi wote wa Mkoa huo  kuwa serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi imeanza kulifanyia kazi ombi lao la kuwezeshwa halmashauri za mkoa huo kupimiwa ardhi kwa ajili ya wawekezaji.

Aidha, kuhusu ombi la kuvirudisha serikalini viwanda vya Nyuzi Tabora, kiwanda cha maziwa na kile cha misitu alisema kuwa litafanyiwa kazi na kama watapatikana wawekezaji wenye nia na uwezo mkubwa wa kuviendeleza wapatiwe.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama aliwataka watendaji wa serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali wachape kazi kwa bidii, kujituma na kuwa wazalendo.

Alisema kuwa sekta ya kilimo ikitumiwa vizuri ni  chachu kubwa ya kukua kwa uchumi wa taifa kwani nchi kama China,India,Brazil,Indonesia na Vietnam zimefanikiwa sana kupitia sekta hiyo kwa kufanya kilimo bora cha biashara.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki na Naibu wake, Hussein Bashe waliwataka wakazi wa Mkoani huo kubadilisha mawazo yao na kuwa na fikra za kuwekeza kifaida badala ya kufikiria uwekezaji ambao hauna tija na mashiko huku wakiwataka Watendaji
wa serikali kuacha ukilitimba bali wawaongoze wananchi vizuri.

Walishauri kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata mazao ya wanyama na viwe endelevu na kuboreshwa malighafi zinazozalishwa kwa ajili ya wawekezaji pia waliwataka kuacha tabia ya kuwa na mifugo mingi isiyo na faida bali wafuge kisasa ilikuwa na mifugo bora itayokidhi ushindani wa masoko.

Awali, Mkuu wa Mkoa huo alieleza wametenga jumla ya hekta milioni 1.36 kwa ajili ya uwekezaji na kubainisha kuwa mkoa una fursa nyingi ambazo zinaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi hivyo akatoa wito kwa wawekezaji kuzichangamkia huku akitaja kauli mbiu yao kuwa ni ‘Wekeza Tabora kwa uchumi wa kijani’.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Geita, Katavi, Mara na Kigoma pamoja na wadau mbalimbali kutoka Mashirika naTaasisi za kifedha, madhehebu ya dini na wakuu wa taasisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles