27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wa mahakama waaswa kutumia mfumo wa TEHAMA

Na Allan Vicent, Tabora

WADAU wa Mahakama nchini wametakiwa kuweka mifumo ya kidigitali katika taratibu za utendaji wao ili kurahisisha mawasiliano ikiwemo kubadilishana taarifa na mifumo ya mahakama ili kuongeza ufanisi.

Rai hiyo imetolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Jaji Amour Khamis alipokuwa akihutubia wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika Kimkoa jana mjini hapa.

Alisema kuwa ili wananchi waweze kunufaika na huduma za mahakama ambazo sasa zinatolewa katika mfumo wa kidigitali, kila taasisi inayojihusisha na utoaji huduma kwa umma kupitia mahakama inapaswa kuwa na mfumo huo ili kuwarahisishia wananchi.

Alibainisha kuwa ushirikiano wa wadau ni muhimu sana katika kufikisha mawasiliano kwa jamii kwa haraka na uwazi ikiwemo kuwaondolea usumbufu, Mahakama peke yake haiwezi kufanikiwa pasipo kushirikisha wadau.

Jaji Khamis alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania imeendelea kuboresha miundobinu na utendaji wake ikiwa ni sehemu ya mikakati yake kuelekea kwenye Mahakama Mtandao ili kurahisisha utoaji maamuzi na haki kwa wakati.

“Mahakama imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kutoa maoni au mapendekezo kwa kupiga simu au ujumbe mfupi kupitia namba 0752 500 400, utaratibu huu ni mzuri sana utumieni,” alisema.

Akitoa salamu za serikali Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dk. Batilda Burian aliwataka wadau wa mahakama kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayoendelea kufanywa na Mahakama hapa nchini ili kutokwamisha utendaji wake.

Aidha aliwataka kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Maofisa na Watumishi wote wa Mahakama ili kufanikisha utekelezaji wa mipango mikakati ya chombo hicho.

Katika kuunga mkono maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa na serikali kwenye chombo hicho chenye dhamana ya kutoa haki kwa jamii Ofisi yake ilitoa mchango wa runinga 2 na komputa mpakato (laptop) 2 kwa Mahakama hiyo.

Jaji Khamis alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa msaada huo na kubainisha kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha mifumo yao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa manufaa ya jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles