24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wa Bima watakiwa kushirikiana

NA SIDI MGUMIA, Dar es Salaam

KAMISHNA wa Bima Tanzania, Dk. Mussa Juma, amewataka mawakala wa sekta hiyo kushirikiana ili kufanikisha malengo ya serikali. 

Dk. Juma aliyasema hayo jana wakati akifungua rasmi warsha ya siku mbili ya mawakala wa Bima, Tanzania iliyofanyika kwenye ukumbi wa Anatoglo, jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Bima Tanzania, Mussa Juma akimkabidhi zawadi Kamisha wa Bima Mstaafu, Israel Kamuzora.

Alisema katika kufikia malengo haya ni jukumu la mawakala, madalali na wadau wote wa makampuni ya bima nchini kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu ya bima ili  kuuza bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya watanzania na kukabiliana na changamoto wanazopata wateja pindi wanapopata majanga.

Dk. Juma alisema, hii ni semina elekezi ya Mawakala wa Bima Tanzania kwa ajili ya kuwapa ujuzi utakao wasaidia kufanya shughuli zao vizuri.

“Serikali ina mpango mkakati wa miaka 10 na miaka mitano kufikia malengo katika sekta ya fedha hasa kwenye eneo la bima. 

“Malengo hayo ni pamoja na kufikia asilimia 80 ya uelewa ili hadi kufikia mwaka 2030, asilimia 50 ya watanzania wote wawe na bima angalau moja,” mesema Dk. Juma.

Aliongeza, katika kufikia malengo haya ni jukumu la mawakala, madalali na wadau wa makampuni ya bima mbalimbali kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu ya bima na kuuza bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya watanzania.

“Semina hii ni muhimu sana kwa yeyote anayeshughulika na utoaji wa bima, mawakala wakiwa miongoni mwao. Ni elimu ambayo itawaongezea ujuzi wa kuweza kuangalia ‘Agency’ zao, ambazo zitawasaidia kuuza bima na kuwahudumia wateja na hatimaye kusaidia kulipa madai ambayo wateja wao wanakutana nayo,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya bima ya HIA Insuarance Agency, Kizito Jilangi, alieleza namna walivyopambana hadi kufikia malengo yao.

Alisema wao wamefanikiwa kuwa moja ya kampuni ya uwakala zinazofanya vizuri nchini Tanzania kwa kuweka misingi imara sambamba na kuchagua uongozi mzuri.

Jilangi alisema kuwa walihakikisha wanajenga timu bora zilizokuwa na jukumu la kuwahudumia wateja, pamoja na kutafuta makubwa na madogo.

Aliongeza kuwa waliweza pia kuweka malengo ya miaka miwili, mitano na kumi nayo iliwaongoza, na katika hili walikubali kutumia muda na pesa ili wafanikishe malengo yao. 

“Tumefanikiwa kwa sababu tulijaribu kuchukua malengo ya mtu mmoja mmoja ambayo tuliyachanganya na yale ya kampuni, hatua hiyo ilimfanya kila mmoja kujiona anajukumu katika eneo lake,” amesema.

Kamati tendaji ikiwa katika picha ya pamoja na Kamishna wa Bima Mussa Juma.

Pamoja na hilo, alisema walikuwa makini katika kuzifuata sheria za nchi, miongozo mingi waliipata kwa Kamishna wa Bima na timu yake ambaye walimshirikisha kwenye mikakati yao na hii ni kwasababu hawakukata tamaa walipokutana na changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati tendaji ya Umoja wa Mawakala wa Bima Tanzania, Chuki Shaban alisisitiza juu ya suala zima la nidhamu katika kazi za uwakala na kusema kuwa ili wakala aweze kutoa huduma stahiki anapaswa kumjali mteja, kutimiza majukumu yake kwa wakati lakini pia kufuata taratibu muhimu pamoja na sheria za nchi.

Akizungumzia umuhimu wa warsha hiyo, Violet Shaban ambaye ni wakala wa Bima, alisema kuwa hilo ni jambo la msingi sana kufanywa na umoja wao kwani ni vyema kupata wakati wakukumbushana lakini pia kufundishana pamoja na kuelekezana mambo ya muhimu yanayohusu bima kwa ujumla. 

“Natarajia kujifunza mambo ya msingi ambayo yatakuwa na manufaa makubwa kwa kazi zangu za bima.”

Warsha hiyo iliyowahusisha mawakala kutoka mikoa mbalimbali nchini, inatarajiwa kumalizika leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles