27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 7, 2022

Contact us: [email protected]

WADAU JITOKEZENI KUIUNGA MKONO RT

Na JENNIFER ULLEMBO

RIADHA ni moja ya michezo inayopendwa duniani kwa asilimia kubwa, kwani mbali na kuwapa watu fedha kwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, pia umekuwa ukisaidia kuimarisha na kutunza afya.

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) lilianzisha mpango wa kuandaa mashindano katika baadhi ya mikoa kwa kuzingatia kanda mbalimbali, ili kuleta sura ya nchi nzima katika mashindano ya Taifa.

Mpango huo ulifanikiwa na ikaweza kupatikana timu ya taifa iliyoweza kuliwakilisha taifa katika Mbio za Nyika zilizofanyika Kampala, Uganda Machi 26, mwaka huu.

Licha ya Tanzania kutofanya vizuri katika mashindano hayo, bado wanariadha na viongozi wa RT waliendelea kujipa moyo wa kuhakikisha mchezo huo unasonga mbele na kurudisha hadhi yake ya miaka ya nyuma.

Lakini hivi sasa upepo umeonesha kubadilika kwa chama hicho kuandamwa na madeni na kujikuta kikishindwa kufanikisha baadhi ya mipango ya kuendeleza timu ya taifa.

Michezo kama riadha na mingineyo midogo midogo  inashindwa kupewa uzito mkubwa kama ilivyo kwa soka, jambo ambalo kwa upande mmoja au mwingine vyama vya michezo vinajikuta vikishindwa kupiga hatua.

Inaonyesha wazi nguvu za ziada zinahitajika kuiwezesha RT kufanikisha malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu na miaka ijayo.

Umoja na nguvu baina ya viongozi wa chama hicho pekee, haiwezi kuwa njia ya kuusaidia mchezo wa riadha Tanzania kuinuka.

Bado wadau na wapenzi wa michezo nchini wameendelea kuweka uzito kusaidia mchezo huu kusonga mbele.

Nchi yetu imebarikiwa kuwa na vipaji vya wanariadha vijana, lakini kama watakosa misingi na msimamo imara wa kuendeleza kile walichonacho, daima tutaendelea kuwa wasindikizaji katika mashindano kwa shuhudia mataifa ya wenzetu yakibeba medali na kuweka rekodi bora zaidi.

Hivi sasa tunajivunia mwanariadha Felix Simbu, ila ukweli tunatakiwa kutengeneza wanariadha wengine wengi watakaoweza kupokea kijiti cha Simbu, ambaye kwa siku za karibuni ameonekana kuliwakilisha vema taifa ndani na nje ya nchi.

Wadau wa michezo ungeni mkono jitihada hizi za RT kwa ajili ya kuitangaza nchi kupita mchezo huu, ambao miaka ya nyuma ulifanya vema kimataifa kupitia wanariadha Filbert Bayi na Selemani Nyambui.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,670FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles