Wadaiwa sugu waondolewa nyumba za TBA

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital 

 Wakala wa Majengo nchini  (TBA), imeanza kuwaondoa wadaiwa sugu 118  waliopanga  katika nyumba zao za Dar es Salaam, huku zoezi hilo likitarajia kuendelea kwa wiki tatu. 

Hatua hiyo inatokana na wadaiwa hao kushindwa kulipa kodi na kusababisha deni kufikia sh. bilioni 1.1.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 29, 2023,  jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja waTBA wa mkoa huo Benard  Mayemba amesema  Dar es Salaam wana  jumla ya nyumba 1200 na katika nyumba hizo wadaiwa sugu ni 118 ambao  wanadaiwa sh. bilioni 1.1.

“Hivi karibuni Mtendaji Mkuu  wa TBA alitoa rai na taadhari ya namna bora ya kuwekeza na kuwaondosha wapangaji sugu katika maeneo yetu ambao walipewa fursa ya kukaa lakini wamekuwa wakaidi. 

 “Kwa mujibu ya maelekezo ya Mtendaji Mkuu zoezi hili lilipaswa kuanza Disemba Mosi,mwaka huu  lakini kwa mkoa wa Dar es Salaam zoezi rasmi limeanza leo  kwa maana  utoaji notisi kupitia dalali  wa mahakama  limefanyika kwa zaidi ya siku nane hadi kumi zilizopita,’’amesema Mayemba .

 Amesema kutokana na zoezi la utoaji notisi kuisha muda mrefu, hakukuwa na haja ya kusubiri hadi Disemba  kuanza kuwaaondosha wadaiwa wote sugu ambao ni watimishi wa serikali.

 Ameongeza kuwa baadhi ya watumishi hao wamekuwa na tabia ambayo sio rafiki za kiutumishi na kulimbikiza madeni. 

 “Moja ya hatua ambazo zimechukuliwa moja kwa moja kupitia dalali wa mahakama ni kuanza zoezi hili ambalo litachukua takribani wiki tatu na halitaangalia sura, rika wala wadhifa wa mtu yoyote,’’ amesema.

 Amesema yoyote anayedaiwa deni kimsingi anapaswa kupisha nyumba ili wapate fursa ya kupangisha watu wengine.

 “Uendeshaji wa zoezi hili linatupelekea sisi TBA kuweza kupata fedha mbalimbali ambazo zitaweza kufanya ukarabati wa majengo na kuboresha miundombinu ya majengo na kujenga makazi mengine,’’amesema.

Aidha amesema kumekuwa na chagamoto kubwa ya makazi katika mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya hivyo wataweza kurahisishia wakala kuendeleza majengo. 

Kwa mujibu wa taarifa  aliyoitoa Mtendaji Mkuu wa TBA hivi karibuni,  Daud Kondoro, amesema wakala inadai zaidi ya sh.bilioni 7.8 za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba na zaidi ya sh.bilioni 3.5 ni madeni ya taasisi mbalimbali za serikali.

“Deni la shilingi  bilioni 7.8 ni la mwaka wa fedha uliopita hivyo kwa sasa TBA imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai.Moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa mahakama ambaye ndiye amepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA,”amesema.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto  kwa baadhi ya wapangaji kutolipa kodi ya pango kwa wakati hali inayosababisha kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni huku baadhi wakiamini nyumba hizo ni mali ya umma hivyo hawawezi kutolewa hata wakiwa na madeni makubwa.

Kondoro amesema hali hiyo imekuwa kikwazo katika juhudi za kutekeleza mipango yao ya maendeleo kama kufanya ukarabati wa nyumba zilizopo na kujenga nyumba mpya ambazo zitapangishwa au kuuzwa kwa watumishi wa umma.

Amesema   Dodoma, Arusha,Mwanza na Mbeya ndiyo inaongoza kwa kuwa na deni kubwa la kodi ya pango la sh. bilioni 1.4

Aidha amesema kwa sasa tayari kampuni ya udalali wa mahakama iitwayo Wins Auction Mart imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa na hatua hiyo itaanza Desemba Mosi, mwaka huu, kwa nchi nzima.