Na Sheila Katikula, Mwanza
Serikali imewataka wamiliki waliopewa hati za madai ambao hawajatekeleza wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi walipe lasivyo watafikishwa mahakamani awamu inayofuata ili waweze kutekeleza wajibu huo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Naibu Kamshina wa Ardhi Mkoa Mwanza, Elia Kamihanda, amesema Serikali imeweka jitihada za kutoa elimu kupitia kwa watendaji wake wa sekta hiyo na viongozi wa Wizara wamekuwa wakiongoza jukumu hilo sanjari na kusisitiza wananchi kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi.
Ameogeza kuwa hadi sasa jumla ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi mkoani hapa 736 wamepandishwa kizimbani juzi katika Mahakama ya wazi inayoendelea katika viwanja vya michezo vya Nyamagana jijini Mwanza.
Amesema wadaiwa hao wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 3.3 ambao wanatoka kwenye Wilaya nne za jijini hapa za Magu, Nyamagana, Ilemela na Misungwi.
“Tunaanza na mashauri 736 kwani hati za madai ya kodi ya ardhi zilizotolewa siyo hizo 736, tumesambaza hati za madai nyingi sana zinazofika 11,000 kwa wamiliki mbalimbali katika halmashauri za Mkoa huu wa Mwanza.
“Tumeanza rasmi kuchukua hatua ya kisheria ya kuwafikisha mahakamani wamiliki wote wa ardhi ambao ni wadaiwa sugu wa madeni ya kodi ya pango ya ardhi kwani serikali imesisitiza wananchi watekeleze wajibu wao wa kisheria wa kulipa Kodi,” alisema.
Ameongeza kuwa kabla ya kufikia uamuzi wa kuwafikisha mahakamani wamechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwaelimisha na kuwakumbusha kwa kuwapatia ilani na hati za madai ya kodi ya ardhi.
“Kwa sababu hawajawa tayari kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi hiyo Serikali kupitia kwa Kamishina wa ardhi msaidizi Mkoa wa Mwanza kwa viwanja vinavyomilikiwa na mkoa tumeamua kuchukua sheria kwa kuwafikisha mahakamani,” alisema Kamihanda.