31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wadai corona imetoa fursa ya soko mazao ya mikunde

Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Mazao ya Mikunde Tanzania (TPN), umesema msimamo wa Serikali wa watu kutokukaa ndani (lockdown) kutokana na virusi vya corona, umekuwa na manufaa kwao ambapo mauzo ya bidhaa hizo yameongezeka.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam na Mtatibu wa TPN Taifa, Zirack Andrew.

Alisema uamuzi wa Serikali umesaidia sekta hiyo kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine.

Andrew alisema kutokuwekwa kwa zuio la kutoka nje kumesaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mikoani kwenda maeneo ya bandari, viwanja vya ndege, na mipakani tayari kwa kuuzwa nje.

“Tunaishukuru Serikali kwa namna ilivyosimamia suala la corona, imesaidia Tanzania kufanya vizuri kwenye biashara hii ya mikunde, hii yote ni kutokuwapo kwa lockdown, hata wafanyabiashara wanaouza bidhaa nje ya nchi hawakupata usumbufu katika kupata huduma za bandari ya Dar es Salaam.

“Hii ilisaidia Tanzania kuuza mazao ya karibu dola za Marekani milioni 70 kwa Januari hadi Mei mwaka huu, hivyo tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi huo iliochukua, umesaidia kuokoa uchumi wa wakulima wengi,” alisema Andrew.

Akitolea mafano nchi jirani ya Kenya, Andrew alisema vikwazo vya usafiri vilivyowekwa nchini humo viliathiri mauzo ya kilimo hatua mbayo iliwalazimu wakulima kuacha mazao yao shambani.

“Hata hivyo kwa hapa kulikuwa na madhara machache kwa wafanyabiashara, hususan wale wanaouza bidhaa hiyo kwenye taasisi mbalimbali zikiwamo shule na vyuo.

“Pia kumekuwa na kusuasua kwa taasisi za kifedha kukopesha makampuni yanayouza mazao nje ya nchi kwa kuhofia kupungua kwa soko la kimataifa,” alisema Andrew.

Mshauri wa Sera na Mipango wa TPN, Junior Ndesanjo, akizungumzia changamoto inayoikabili wakulima, alisema mvua zilizonyesha zaidi ya kipimo zimeathiri kwa sababu mazao mengi ya mikunde yaliharibikia shambani.

“Bei ya mwaka jana pia ilichangia kuwavunja moyo wakulima na kuwafanya kutoongeza maeneo ya uzalishaji. Pia kupungua kwa uzalishaji kumesababishwa na ugonjwa ulioshindwa kutambulika kwa mazao ya mikunde kwenye mikoa kama Manyara.

“Aidha, soko la kimataifa linatoa ishara ya kuimarika msimu huu kwa sababu intelijensia yetu inatuonyesha kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa dengu nchini India kutokana na uzalishaji kuwa mdogo, hiyo inaweza kutengeneza soko kubwa la dengu za Tanzania, hasa tukizingatia kuwa soko la India kwa mazao haya litafunguliwa Septemba na Oktoba,” alisema Ndesanjo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles