30.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Wachina wachefukwa hospitali kujengwa mithili ya choo

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

JENGO la hospitali moja kubwa nchini China linaweza kuwafanya watu wengine wacheke kidogo.

Jengo la hospitali hiyo ya Kimataifa ya Tiba Guangxi Zhuang, iliyopo Jiji la Nanning nchini humo limejikuta likipata umaarufu mbaya.

Limebatizwa kila aina ya majina mabaya na machafu ya kejeli katika mitandao ya jamii.

Sababu ya kulifanya likabiliwe na kila aina ya maneno ya kebehi ni mwonekano wake.

Jengo hilo lililoenda hewani lililopo kusini mwa China linaonekana kutowafurahisha Wachina waliolishuhudia kwa macho au walioliona mtandaoni baada ya kurushwa na walioushuhudia; limepewa jia la choo kikubwa.

Kwa mujibu wa mtandao wa Yahoo, jengo hilo lenye umbo la choo linachukua eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 187,500 katika Hospitali ya Kimataifa ya Guangxi Zhuang.

Licha ya kwamba ukiliangalia kwa haraka bila kuwa na fikra zozote kichwani kwako unaweza usiuone mfanano huo wa choo, lakini ukitulia utauona wazi.

Jengo hilo lenye rangi ya njano limeundwa na sehemu mbili zilizochangia mfanano huo kukamilika.

Sehemu ya kwanza ni nusu duara, ambapo eneo lilipokatizwa, duara limesimamishwa. Sehemu ya pili ni pale ambapo jengo limeenda juu hewani na hivyo kwa pamoja kutengeneza umbo la choo cha kukaa.

Katika jengo la hospitali hiyo inayobezwa na watu wengi, sehemu yenye ghorofa nyingi ina umbo la tangi la maji kama la choo, huko ndiko wagonjwa wanapolazwa.

Sehemu ya nusu duara inayofanana na sehemu ya kukaa ya choo, ndipo palipo idara mbalimbali za hospitali hiyo.

“Ubunifu huo unahusishwa na majukumu ya hospitali hiyo,” anasema mkazi wa Nanning, Chaoyu Feng, kwa njia ya video iliyorushwa na mtandao wa India Today.

“Kwa mtazamo wangu si umbo baya, pengine linawafaa na kuwapendeza wagonjwa. Wakati inaponyesha mvua nje, mgonjwa anaweza kwenda katika idara yoyote ile bila kulazimika kutumia mwavuli,” anasema Feng.

Anaongeza kwamba muundo wa hospitali hiyo unamanisha matumizi sahihi ya ardhi.

Licha ya kwamba inaweza kuonekana  watumiaji wa mitandao nchini humo wanafanya mizaha tu wanapokejeli jengo hilo, ukweli ni kwamba hawatanii bali wanamaanisha kile wanachokisema.

Serikali ya China inafahamu fika fikra za Wachina pindi linapokuja suala la majengo ya ajabu ambayo yametawala nchini humo.

Februari mwaka jana, Serikali ya China ilipiga marufuku ujenzi wa majengo yenye maumbo ya ajabu hasa yanayoonekana kama kioja au kukosa heshima.

Uamuzi huo ulikuja baada ya watu kulalamikia muundo wa jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Beijing, linaloonekana kama sehemu za siri za kike huku la makao makuu ya gazeti la People’s Daily likiwa katika umbo la sehemu za siri za kiume.

Hata hivyo, kwa sababu zisizojulikana maumbo ya majengo yanayofanana na choo yameachwa bila kuguswa na amri hiyo.

Mbali ya jengo hilo la hospitali ya kimataifa, pia kuna la Chuo Kikuu cha Henan nalo lina mwonekano wa choo.

Awali watu walilalamikia jengo hilo la chuo kikuu, wakisema mbunifu wa ramani alifanya makusudi lionekane muundo huo badala ya taswira nyingine ya kuheshimika.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,464FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles