MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Wachina wawili kulipa faini ya Sh bilioni 108 au kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na vipande 728 vya meno ya tembo bila kibali.
Pia mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa magari matatu ya washtakiwa hao mawili yakiwa aina ya Noah yaliyodaiwa kutumika kubeba meno hayo.
Akitoa hukumu hiyo mahakamani hapo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyporiani Mkeha, alisema washtakiwa hao wametiwa hatiani katika mashtaka mawili kati ya matatu yaliyowakabili ambayo ni kukutwa na meno hayo bila kibali na kujaribu kutoa rushwa ya Sh 30,250,000 kwa askari walioenda kuwakamata.
“Katika shtaka la kukutwa na meno hayo bila kibali, kila mshtakiwa atatakiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya shilingi 54,358,650,000,” alisema Hakimu Mkeha.
Alisema kwa shtaka la kujaribu kuhonga askari, kila mshtakiwa ametakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja au kwenda jela miaka mitano na adhabu hiyo itakwenda pamoja.
Alisema amezingatia hoja za pande zote mbili lakini kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hasa jinsi nchi inavyopoteza idadi ya tembo na hasara iliyopatikana.
“Hii ni kesi inayostahili kutolewa adhabu ya kiwango cha juu kulingana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhika kwamba upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa na washtakiwa hawakuweza kuwajibika ipasavyo kuutia matundu ushahidi wa upande wa mashtaka,” alisema Hakimu Mkeha.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana washtakiwa hao wanatiwa hatiani kwa makosa hayo mawili.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao kwa sababu kitendo chao kimesababisha kuuawa kwa takribani tembo 226.
Nchimbi alisema inaonekana washtakiwa hao walikuwa vinara wa vitendo hivyo vya ujangili kwa kuwa tangu wakamatwe hakujatokea watuhumiwa wengine kukamatwa na idadi kubwa ya meno ya tembo kama wao tangu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014.
“Watuhumiwa hawa hawahitaji huruma ya mahakama kwa kuzingatia ukubwa wa kosa walilotenda, tembo waliouawa ni sawa na robo ya idadi ya tembo 892 wanaodaiwa kuuawa nchini kuanzia mwaka 2012 hadi 2013 na kwa mujibu wa takwimu za taifa wanyama hawa kama wangekuwepo taifa lingeingiza pato lake katika sekta ya utalii,” alisema Nchimbi.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Nehemia Nkono, aliiomba mahakama hiyo iwahurumie washtakiwa hao kwa kuwa ni wakosaji kwa mara ya kwanza huku akikanusha kuwa wao ndio vinara wa vitendo vya ujangili.
Washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 2, 2013 katika Mtaa wa Kifaru uliopo Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam. Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walikutwa na vipande vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 1,880 ambavyo vina thamani ya Sh 5,435,865,000 na walivimiliki bila kibali cha Serikali.