30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wachimbaji wa Tanzanite waweka matumaini yao kwa Magufuli

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

CHAMA cha wachimbaji wa madini Mkoa wa Manyara (Marema) kwa kushirikiana na Kamati ya Madini ya Tanzanite, wamempongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kuchaguliwa kwa awamu nyingine.

Aidha wamemuahidi kuhakikisha sekta ya madini nchini inakua kwa kasi kwa kulipa kodi stahiki pamoja na kuzuia utoroshwaji wa madini hasa ya Tanzanite ambayo yanachimbwa eneo moja duniani la Mirerani, Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa Marema, Justine Nyari, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema wanampongeza Rais Dk. Magufuli kwa kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu, ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya utawala wake amesaidia kukuza sekta ya madini ikiwemo Tanzanite.

“Watanzania wamethibitisha kazi aliyofanya katika miaka mitano iliyopita ni kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini,”alisema Nyari

Mwenyekiti huyo alisema moja ya alama kubwa aliyoacha katika uongozi wake wa awamu ya tano katika sekta ya madini ni pamoja na ujenzi wa ukuta kuzunguka machimbo hayo ya Mirerani ambao umesaidia kuondoa utoroshwaji wa madini hayo.

“Madini hayo awali baadhi ya wachimbaji walikuwa wakiyatorosha, ila ukuta umesababisha dunia imeamini Tanzanite inatoka Tanzania na inadhibitiwa kwani vyombo vyake na Wizara ya Madini wamekuwa wakidhibiti madini yale yanapotoka na wachimbaji wamekuwa na imani kubwa na baada ya tathmini na kulipa kodi ya serikali wanasafirisha madini yao,”alisema

“Lingine tunalompongeza nalo ni kuondoa kodi ambazo zilikuwa ni kero kwa wachimbaji wadogo,madini yameongezeka baada ya kodi kufutwa na mapato yamekua,masoko ya madini nchi nzima nayo yamechangia wafanyabiashara kuwa na uhakika wa masoko yao,”aliongeza.

Nyari alisema wanaamini miaka mitano ya uongozi wa awamu ya pili ya Dk. Magufuli wanatarajia changamoto mbalimbali zilizobaki zitafanyiwa kazi ili kuendelea kukuza sekta hiyo.

Alitaja baadhi ya changamoto ni pamoja na matatizo ya vifaa vya kuchimbia madini ikiwemo milipuko ambayo inaletwa nchini na kupelekwa kwa wachimbaji wadogo ambapo baadhi yao wanashindwa kumudu gharama.

“Naamini Rais kwa kushirikiana na watendaji wengine ikiwemo TRA (Mamlaka ya Mpato Tanzania), watapunguze baadhi ya kodi za milipuko ili wachimbaji wanunue kwa urahisi na wachimbe kwa wingi ili madini yanayopatikana yawe mengi na kodi iongezeke badala ya ile ya kwenye vifaa,”alisema

“Mfano kibali cha kununua vifaa vya uchimbaji labda kampuni ziko tatu unapewa kibali kimoja ambacho gharama yake ni Sh. 100,000 na kinaisha muda wake ndani ya mwezi mmoja na ikiisha kama hujatumia huwezi kutumia tena,”aliongeza

“Lakini unakuta labda mafuta ya baruti yako kwenye kampuni X, lakini umepewa kibali kwenda kampuni B, ukienda kwenye kampuni B ukakosa yale mafuta kile kibali hakiwezi ku apply kwenye kampuni X.

“Ni ushauri wangu kwamba kibali kitolewe kiandikwe kampuni X/B ili ukikosa kifaa kimoja katika kampuni ili kibali kikuwezeshe kwenda kampuni nyingine,”alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Madini aina ya Tanzanite Tanzania, iliyopo chini ya Shirikisho la Vyama vya wachimbaji wadogo wa madini Tanzania (FEMATA), Nene Lyimo, alisema wakiwa kama wadau muhimu wa maendeleo wanampongeza Rais Magufuli na kuahidi kuendelea kukuza uchumi kwa kulipa kodi stahiki.

“Tunampongeza kwa ushindi na tuna imani naye na tuna matarajio makubwa zaidi hasa kwa sisi wachimbaji kiukweli tumenufaika na uongozi wake sasa hivi Tanzanite imeshuhudiwa tumempata bilionea Laizer.

“Siku za nyuma haikuwahi kupatikana madini ya hivyo na hata kama yalipatikana yalitoroshwa,ukuta umesaidia sana na utakuza sekta hii na tunamuahidi kukuza sekta ya tanzanite na kuongeza wigo wa walipa kodi wengi.

“Wachimbaji na watanzania wenzangu kwa ujumla uchaguzi umekwisha tunamuahidi Rais kuchapa kazi,ili tuboreshe maisha yetu na kukuza uchumi wa kati ili tufike uchumi wa juu zaidi,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles