29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wachimbaji madini Simiyu wataka Ofisa aondolewe

Na Delick Militon, Simiyu

Wachimbaji wadogo katika mgodi wa dhahabu Bulumbaka namba mbili, ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wametaka kuondolewa kwa Ofisa Madini wa Mkoa huo, Joseph Kumbulu.

Mbali na wachimbaji hao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo, kimetoa muda wa siku tano kwa viongozi wa Serikali kuhakikisha wanatatua malalamiko ya wachimbaji hao dhidi ya Ofisa madini huyo, huku kikitaka aondolewe.

Baadhi ya wachimbaji

Katika Mkutano wao na Kamati ya ulinzi na usalama, Kamati ya Siasa Wilaya, wachimbaji hao wamemtuhumu Ofisa Madini huyo kwa kuendesha vitendo vya unyanyasaji dhidi yao ikiwa pamoja na kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wa mgodi huo na kusababisha uzalishaji kushuka.

Wamesema Ofisa Madini huyo amekuwa akiwakamata wachimbaji mbalimbali kila mara na kuwaweka ndani kisha kuwataka watoe pesa ndiyo waweze kuachiwa ambapo wengi wao ufanya hivyo.

“Alitukamata wachimbaji zaidi ya 12, tukawekwa ndani siku tatu, huku akitutaka kutoa Sh 500,000 kila mmoja ndiyo tuweze kutoka, wote tulifanya hivyo, tukatoa hizo pesa ili tuachiwe na hatukupewa risiti,” amesema Jemsi John.

Aidha, wachimbaji hao wameeleza kuwa, Ofisa madini huyo amekuwa akikataa kufanya mgao wa mawe, tofauti na zamani ambapo utaratibu ambao ulikuwepo ulikuwa ukifanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa lakini kwa sasa mgao unafanyika mara moja kwa wiki.

Wamesema kuwa mbali na hilo, hali zao za kifedha zimekuwa ngumu kwani Ofisa Madini huyo amebadilisha utaratibu wa mgao: ….“Uko nyuma kuna baadhi ya mifuko walikuwa wakipewa wachimbaji ili kurahisisha uzalishaji lakini yeye ameondoa hilo,” amesema Denis Clementi

“Ofisa Madini huyu alikuja na wahasibu wake kutoka uko Shinyanga alikotolewa, wahasibu hao wamekuwa wanyanyasaji sana, wanakamata watu ovyo, lakini tumewadai risiti za EFD wao wanatupatia za karatasi…tukilalamika wanatuweka ndani,” amesema Denis Philimon.

Wameeleza kuwa wamekuwa wakimuita Ofisa Madini huyo kwa ajili ya kufanya kikao na kutatua changamoto mbalimbali lakini amekuwa akigoma na kusema yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho na hakuna kiongozi yeyote wa kuwasaidia hapa nchini.

Upande wake, Daniel Rubeni amesema kuwa; “Amekuwa akitutishia kuwa yeye ni usalama wa taifa, yeye ndiye mwenye kauli ya mwisho na hakuna kiongozi yeyote wa serikali mwenye mamlaka dhidi yake, mtu ukisikika unaongea ongea sana unakamatwa na kuwekwa ndani.

“Kama wachimbaji tunaiomba serikali watuondolee huyu mtu, hatumtaki wachimbaji, ametufanya kuwa maskini,uzalishaji umepungua, amekuwa na kiburi hataki kutusikiliza, vitendo vya unyanyasafi vimedhidi, amekuwa kero, wachimbaji hatuna amani, hatumtaki,” amesema Ruben

Nao wamiliki wa mashamba wamesema kuwa wamekuwa katika wakati mgumu tangu Ofisa Madini huyo ameletwa, ambapo amekuwa akitumia pesa kuwanyanyasa baadhi yao ambao wamekuwa wakigoma kuruhusu uchimbaji kuendelea.

Kufuatia kukithiri kwa malalamiko hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya, Juliana Mahongo, ametoa muda wa siku tani kuhakikisha malalamiko hayo yanatatuliwa, huku Katibu wa chama hicho Wilaya Mwajemi Balagama akiungana na wachimbaji hao kutaka Ofisa huyo kuondolewa.

“Sisi Chama tunasikitika sana kwa hali hii, huyu Ofisa Madini amekuwa na dharau kubwa, anaitwa hata kwenye vikao vikubwa vya viongozi Wilaya lakini anagoma, leo kwenye huu mkutano ameitwa amegoma, huyu hatufai,” amesema Mahongo.

Upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga, amesema Ofisa Madini huyo amekuwa na kiburi, kwani kila wanapomuita kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama amegona kufika huku mara ya mwisho akataka kupatiwa ajenda kwanza kabla ya kufika kwenye kikao.

Aidha, Kiswaga amepiga marufuku wahasibu hao waliolalamikiwa kukanyaga kwenye mgodi huo, huku akizuia kukamatwa kwa watu ovyo ovyo kabla ya ofisi yake kupata taarifa na kutoa kibali cha kufanyika kwa zoezi hilo.

“ Ofisa madini huyu amekuwa shida, lakini mimi kama Mkuu wa Wilaya nasema sitakubali, lazima tusimamie maelekezo ya Rais ya kutetea wanyonge, tumemuita mara nyingi lakini hataki, amefanya mgodi huu kama mali ya familia yake,”amesema Kiswaga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles