24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Wachezaji wasikurupuke kusaini mikataba

Mwandishi Wetu

DIRISHA kubwa la usajili kwa ajili ya msimu ujao wa  Ligi Kuu Tanzania Bara, bado halijafunguliwa rasmi lakini baadhi ya klabu tayari zimeingia katika mawindo ya kusaka nyota wa kuwasajili.

Licha ya kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halijatangaza rasmi kuanza kwa msimu mpya wa usajili, tayari baadhi ya klabu zimeanza usajili wa awali kwa lengo la kuboresha vikosi vyao.

Usajili mpya wa wachezaji unatarajia kuanza rasmi baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara ambayo imesalia michezo michache kabla ya kufikia tamati.

Kuanzia hapo, klabu zitahamia katika vurugu za usajili ambazo tayari zimeanza kusikika hasa kwa klabu kubwa zenye ushindani wa soka nchini, Simba na Yanga.

Ikumbukwe kuwa, Ligi Kuu kwa sasa imesimama, baada ya Serikali kupiga marufuku shughuli zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwamo michezo, uamuzi ambao unalenga kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya ugonjwa wa corona, ambavyp vimesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.

Kwa kuwa kipindi kinachokuja ni cha mavuno kwa wachezaji walio wengi hasa kwa wale walioonyesha viwango katika msimu unaomalizika, lakini wanatakiwa kuwa makini na mikataba ya awali wanayokubaliana na klabu zinazowahitaji.

Tumeshuhudia unapofika msimu wa usajili, wachezaji wengi wanakurupuka kusaini mikataba pasipo kujua haki zao na mwisho wa siku wanajikuta wameingia katika matatizo ya kutolipwa.

Mifano ni mengi kwa wachezaji ambao walikurupuka kusaini mikataba kwa kipindi kama hicho kinachokuja na mwisho wa siku  kuwa ni usumbufu mkubwa wa kupata stahiki zao.

Msimu unaomalizika kulikuwa na kesi nyingi za wachezaji kudai fedha zao za usajili kutoka kwa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, ili tatizo hilo lisijitokeze ni vizuri wakawa makini katika kusajili mikataba.

MTANZANIA tunawaasa wachezaji kuisoma kwa umakini mikataba wanayopewa na klabu zinazowahitaji na hata wale wanaoongeza  ili kujua kama yale wanayoyahitaji yamo au la.

Tunakumbusha hilo baada ya kubaini wapo wachezaji ambao kutokana na kuahidiwa kitita kikubwa cha fedha wamekuwa wakipoteza umakini katika kuisoma vizuri mikataba yao, matokeo yake mwisho wa siku hujikuta wakiingia kwenye migogoro isiyo ya lazima na klabu zao.

Wapo wachezaji waliowahi kudai haki ambazo kwenye mikataba yao hazimo, haya yote ni matokeo ya kutoisoma na wakati mwingine kutoielewa mikataba wanayoingia na klabu zao.

Ushauri wetu mwingine, kwakua mikataba mingine uandikwa kwa lugha ya kiingereza ambayo baadhi ya wachezaji  hawaifahamu kwa ufasaha, ni vizuri wakaipeleka kwa wanasheria ili wawatafsirie kipengele kimoja baada ya kingine.

Kwa kufanya hivyo wachezaji wengi  watajua mapema kilichoko ndani yake na kama kuna mapungufu yaweze kurekebishwa mapema ili kila upande uridhie .

Zaidi ya hilo, wachezaji wanapaswa kuangalia mahali sahihi ambako watapata fursa ya kuendeleza vipaji vyao na si kukimbilia katika timu ambazo wanafahamu wao wanakwenda kujimaliza na baada ya muda mfupi hawatahitajika tena. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles