Wachezaji United kumpigania Solskjaer

0
444

MANCHESTER, ENGLAND

MLINDA mlango namba moja wa timu ya Manchester United, David de Gea, amethibitisha kuwa wachezaji wa timu hiyo wameungana kwa ajili ya kumpigania kocha wao Ole Gunnar Solskjaer.

Kocha huyo kwa sasa yupo katika wakati mgumu kutokana na mwenendo wa timu hiyo kuwa mbaya kwenye michuano mbalimbali, huku mashabiki wakianza kuushawishi uongozi uvunje mkataba wake.

Solskjaer alipewa jukumu la kuifundisha timu hiyo Desemba mwaka jana mara baada ya kufukuzwa kwa kocha Jose Mourinho, lakini baadhi ya mashabiki na viongozi wanaonekana kutoridhishwa na uwezo wake.

De Gea ambaye amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu na kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi ndani ya kikosi hicho, amesema watahakikisha wanapambana kila mchezo ili kulinda kibarua cha kocha huyo.

“Solskjaer ni sehemu ya familia yetu, amekuwa hapa kwa kipindi kirefu akiwa kama mchezaji na sasa ni kocha, anaijua vizuri klabu hii na kitu muhimu ni kwamba timu yote ipo chini yake, hivyo tukiwa kama wachezaji lazima tumpiganie hadi hatua ya mwisho.

“Tunaamini ni kocha mwenye uwezo mkubwa ambaye anaweza kutupatia mafanikio, hivyo lazima wachezaji tushikamane na kuwa kitu kimoja hadi mwisho,” alisema De Gea.

Kipa huyo ni mmoja kati ya wachezaji waliopo hapo kwa kipindi kirefu, alijiunga na United tangu mwaka 2011, akiwa amekaa langoni mara 281 kwenye michezo ya Ligi Kuu, lakini kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Septemba 2, mwaka huu, alikuwa anahusishwa kutoka kuondoka na kujiunga na Real Madrid kabla ya wiki kadhaa zilizopita United kumtia kitanzi kwa kumpa mkatana wa pauni 378,000 kwa wiki.

“Hii ni klabu kubwa nchini England, ninajivunia kuwa hapa kwa kuwa ninapewa heshima inayostahili, nimekuwa hapa kwa kipindi kirefu na bado nina furaha kuendelea kuwa hapa,” aliongeza mchezaji huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here