31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WACHEZAJI MSIJIANDALIE MAJUTO MSIMU UJAO WA VPL

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

USAJILI wa Ligi Kuu Tanzania Bara umefunguliwa rasmi Juni 15, ambapo zoezi hili litaendeshwa hadi Agosti 6, mwaka huu.

Ikiwa tayari baadhi ya timu zilifanikiwa kuanza kusajili kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la usajili, tayari vioja vimeanza kuibuka.

Ukweli halisi vita ya usajili VPL haijawahi kumwacha mtu salama, hivyo ndivyo tunavyoweza kusema kutokana na staili ambayo imekuwa ikitumiwa kila msimu.

Staili ya usajili kila mara imegeuka kivutio, kwani viongozi wengine wenye dhamana ya kusajili hujikuta wakiishia njiani kutimiza azma na malengo yao.

Hivi sasa klabu ambazo zimeonyesha kuwa moto katika usajili ni Simba, Yanga, Azam FC na Singida United.

Klabu hizi kwa ujumla kila moja imejiwekea malengo ya kumiliki wachezaji wazuri wenye viwango vya hali ya juu.

Ila linapofika suala la mchezaji kufanya mazungumzo na timu nyingine na kuingia mkataba katika klabu tofauti, daima kinachobaki ni kichekesho.

Tayari kesi za wachezaji kufanya mazungumzo ya awali na klabu ambazo zimeshindwa kuwasajili na kujikuta wakisajiliwa kwingine zimezidi kushika kasi.

Ni vyema viongozi wakawa makini wakati wanafanya maamuzi na kuacha mtindo wa kutamani kumiliki wachezaji wengi ambao mwisho wake wanaishia kusugua benchi.

Kweli mchezaji azungumze na timu flani kwa ajili ya usajili, hapo hapo usikie klabu nyingine imemalizana naye juu kwa juu.

Inaonyesha wazi mchezaji huo hakuwa na mwelekeo na hajui anatakiwa kufanya nini, bali anachokihitaji ni kuona bora liende, ajipatie timu ya kuchezea msimu ujao.

Usajili huu utakuja kugeuka majuto kwa baadhi ya wachezaji watakaoshindwa kutumia vema karama zao kipindi hiki.

Kwa sasa ni vigumu kulijua hilo mapema kutokana na maneno matamu na ahadi lukuki zinazotolewa na viongozi husika, waliobeba jukumu la kusimamia usajili kwenye timu husika.

Tamaa ya fedha imekuwa ikizidi kuwamaliza wachezaji, viongozi kwa ujumla. Kila mmoja amekuwa akivutia upande wake, kwa madhumuni ya kujinufaisha bila kufikiria mbeleni.

Usajili huu utazalisha wachezaji wengi watakaojikuta wakisugua benchi kwa kukosa nafasi katika vikosi vya kwanza, hivyo hivyo utazalisha chuki kwa viongozi kuonekana wamesajili wachezaji magarasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles