WACHANGISHANA FEDHA KUTOA WENZAO GEREZANI

0
852

Na Lupakisyo Kingdom-Songwe


WANANCHI wa Kjiji cha Mfuto, Kata ya Miunga, Tarafa ya Ndalambo wilayani Momba mkoani Songwe, wameamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kukata rufaa ili kuwatoa gerezani Obert Simkonda na Sadoc Schone ambao wamefungwa na mahakama ya wilaya hiyo, kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja kwa kosa la kumjeruhi Zacharia Schone.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo juzi mbele ya Diwani wa Kata hiyo, Godifrey Siame (Chadema), walisema wameamua kufanya hivyo baada ya kutoridhishwa na ushahidi uliotolewa upande wa mlalamikaji na matendo mema waliokuwa nayo vijana hao.

Mmoja wa wananchi hao, Taswilwa Shone, alisema tangu vijana hao wazaliwe hawajawahi kushtakiwa kwa kosa la jinai wala madai.

"Kama mlezi wa hawa vijana, sijawahi kusikia wala kuona wanashtakiwa kwa kosa lolote iwe katika ofisi ya Serikali ya mitaa wala mahakamani," alisema Schone.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chipoma, Tito Simkonda, alisema yeye ndiye aliyempeleka mlalamikaji kutibiwa majeraha katika zahanati ya Mfuto, lakini ushahidi uliotolewa na askari mpelelezi wa kesi hiyo hakuridhishwa nao.

"Mimi ndiye niliyemsaidia huyu mlalamikaji mpaka kumpeleka  zahanati ya Mfuto, lakini ushahidi umetolewa eti alitibiwa Tunduma, wakati tunahukumu kesi hii haikuwa na ushahidi wa silaha aina ya panga ila mahakamani imeletwa, hakuna askari ambaye amewahi kuja katika kitongoji changu kupeleleza," alisema Simkonda.

Kutokana na hali hiyo, Siame aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati wanachangisha fedha hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here