23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wachache wajitokeza uchaguzi Serikali za Mitaa

WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI

WANANCHI katika maeneo mbalimbali nchini, wamepiga kura kuchagua viongozi wao wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, huku baadhi ya maeneo yakikumbwa na changamoto kadhaa ikiwamo idadi ndogo ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa agizo la Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  Seleman Jafo, alilolitoa juzi alisema uchaguzi huo utafanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini isipokuwa mikoa mitatu ya Katavi, Ruvuma na Tanga ambapo wagombea wa CCM walipita bila kupingwa, baada ya baadhi ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo.

Hata hivyo, jana MTANZANIA ilitembelea katika baadhi ya maeneo ya mitaa ambayo uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika ambapo katika Kituo cha Shule ya Msingi Mwananyamala Mchangani Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, hadi kufikia saa nne asubuhi kulikuwa hakuna vifaa vya kupigia kura huku wananchi waliojitokeza wakibaki kukosa la kufanya.

Hata hakukuwa na wasimamizi wa uchaguzi ingawa katika kituo hicho kulikuwa na wapiga kura wasiozidi watatu ambao nao walisubiri na baadaye kuondoka katika eneo hilo bila maelezo.

Mmoja wa wananchi hao alijitambulisha kwa jina la Athuman Said, alisema alifika katika kituo hicho kwa lengo la kupiga kura lakini alijikuta amekaa muda mrefu bila maelekezo, hivyo kuona amenyimwa haki yake ya kuchagua kiongozi anayemtaka.

“Nimekuja kupiga kura hapa Shule ya Mwananyamala, nimefika wa kwanza lakini baadaye wakaja wenzangu wawili, ambao wote tumebaki tumesimama na hatuna wa kumuuliza, nipo hapa tangu saa mbili asubuhi na sasa ninaondoka maana ratiba yangu imevurugwa kabisa,” alisema Said

MTANZANIA ilifika katika Mtaa wa Mikoroshini Kata ya Ndugumbi, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, na kushuhudia idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura kituoni hapo licha ya mvua kuisha.

Pia lilishuhudia wapigakura hao wakihangaika kutafuta majina yao katika ubao wa majina kutokana na majina hayo kutokupangwa kwa kufuata alfabeti.

Ulinzi uliimarisha kwa idadi kubwa ya askari polisi waliokuwa wametanda katika kituo hicho. 

Akizungumza kituoni hapo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni, Kiduma Mageni, alisema uchaguzi huo umeenda vizuri licha ya mvua kuendelea kunyesha wakati wote.

Alisema mtaa huo ndiyo pekee uliofanya uchaguzi kwenye manispaa hiyo ukihusisha wagombea wa vyama viwili vya CCM na ACT Wazalendo, baada ya mitaa mingine 105 CCM kupita  bila kupigwa.

“Uchaguzi unaendelea vizuri hapa kwani wananchi wamejitokeza licha ya hali ya hewa kuwa ya mvua, hapa tunawagombea wa vyama viwili, CCM na ACT Wazalendo, hivyo hadi sasa bado hatujapata changamoto yoyote,” alisema Mageni.

Katika hatua nyingine alipoulizwa juu ya kuwapo kwa mgombea wa ACT Wazalendo licha ya chama chake kutangaza kujitoa kushiri katika uchaguzi huo alisema kuwa mgombea huyo alikidhi vigezo kwa kuwa alidhaminiwa na chama kupitia kwa katibu wake wa tawi.

“Mgombea wa ACT kwanza alitambulishwa na chama chake akaja kuchukua fomu na kisha akarejesha kwa katibu wake wa tawi akadhaminiwa na kurejesha fomu, bila ya kutuambia kwamba amejitoa, lakini pia katibu mwenyewe wa tawi lililomdhani naye hakutuambia kuwa amejitoa.

“Hivyo ukiniambia kwamba alijitoa itakuwa ni kinyume cha utaratibu. Hata unaponiambia kuwa walisema nembo yao isitumike bado sisi katibu wa tawi wa chama hicho hakutuambia, ikizingatiwa kuwa haki ya kugombea ni ya mtu ambaye anatambulishwa na chama ana hata sisi ACT walituambia kuwa mgombea atatambulishwa na katibu wa tawi.

“Kwa mujibu wa kanuni zinaeleza mtu akitaka kujitoa anatakiwa kufuata taratibu, mbona kuna mitaa mingi walifuata taratibu za kujitoa wakajitoa! Pia ikumbukwe kuwa hatumlazimishi mtu kujitoa.

“Kutokuwapo kwa wakala kutoka ACT hakutaathiri chochote sisi tumeapa kiapo cha utii na uaminifu hivyo asipokuwapo kura zake tutahesabu na kujhakikisha zinalindwa,” alisema .

Alisema ikitokea mgombea huyo hatakuwapo kusaini katika matokeo hakuna kanuni inayosema yatabatilishwa.

Mmoja wa wapiga kura mkazi wa mtaa huo, Azizi Ng’amilo alisema changamoto aliyoiona katika uchaguzi huo ni majina kutoandikwa kufuata alfabeti, jambo lililoleta usumbufu wa kupata jina la mpiga kura.

Alisema ametimiza haki yake ya msingi ya kupiga kura kama mwananchi na kuna amani hakuna fujo.

Naye Ofisa Uchaguzi wa Manispaa ya Ilala , Hilary Baina alisema ni kata mbili ambapo Kata ya Kimanga ilikuwa na vituo viwili vya Darajani na Kisima cha Maji  iliyoshirikisha vyama vya CCM na ACT Wazalendo.

“Kata nyingine ni Buguruni ambapo Mtaa wa Malapa ulikuwa na vituo vitatu vya Shule ya Msingi Hekima, Kwa Maumba na Machachuni ukishirikisha vyama vya CCM na ADC, na tunashukuru kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu kwani hakuna tukio lolote baya lililojitokeza,” alisema Baina.

Vijana wajitokeza wachache

Katika uchaguzi wa Serikali  uliofanyika jana Kijiji cha Senani ambacho ndicho kijiji pekee kinafanya uchaguzi kwa Mkoa wa Simiyu,  Mtanzania imeshuhudia idadi kubwa ya wapiga kura ambao wamejitokeza wakiwa wanawake na wazee .

Hata hivyo vijana wameonekana kuwa wachache  ambapo vituo vilifungulia mapema saa 2:00 asubuhi huku baadhi ya vituo wapiga kura wakiwa wachache na vingine vikiwa na foleni.

Akizungumza na waandishi wa habari Msimamizi wa Uchaguzi katika wilaya hiyo, Amina Mbwambo alisema kuwa wananchi wameendelea kufika kwenye maeneo ya kupiga kura kisha kushiriki zoezi hilo.

Alisema kuwa katika kijiji hicho jumla ya vituo vitano vya kupigia kura viliandaliwa vyema pamoja na vifaa vyake, ambapo kipaumbele kilikuwa kikitolewa kwa akina mama wajawazito, wenye watoto wachanga, wazee pamoja na walemavu.

 “Kanuni inasema kuwa mtu ambaye hajui kusoma na kuandika anayo haki ya kutafuta mtu wa kumsaidia, lakini yule anayesaidia hatakiwi kusaidia zaidi ya watu wawili, lakini kutokana na hali ya huku unakuta mtu anasaidia watu hadi watano.

 “Ingawa kanuni inanilinda mimi msimamizi wa uchaguzi, kuruhusu mtu asaidia watu zaidi ya watano, kutokana na kuona idadi kubwa ya wananchi hawajui kusoma, kuandika hata lugha, tumeamua kuwaruhusu watu wawasaidie hata ikizidi mara tano,” aliseka Mbwambo.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga wamesema upigaji kura umepangwa vizuri ambapo wasimamizi na mawakala wanatoa maelekezo kwa wapiga kura bila upendeleo wowote.

HABARI HII IMEANDALIWA NA FARAJA MASINDE Na TUNU NASSOR (DAR),  Derick Milton (SIMIYU).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles