Na Jeremia Ernest, Mtanzania Digital
WABUNIFU chipukizi 15, wameingia katika king’anyiro cha kuwania tuzo ya Emering Designer, inayotolewa kila mwaka katika tamasha la Swahili Fashion Week.
Tuzo hiyo ambayo ilipewa jina la aliyekuwa Mratibu wa Jukwaa hilo marehemu Washington Benbella, ni mahususi kwa wabunifu chipukizi inawapa nafasi ya kushindanisha kazi zao bure katika jukwaa hilo.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo, muasisi wa tamasha hilo Mustapha Hasanali, amesema maombi yalikuwa mengi kumefanyika mchujo na majaji wazoefu wakiongozwa na chifu jaji Jamila Veraswai mpaka kupata wabunifu 15.
“Tulitoa fursa kwa wabunifu kujisajili kuwania tuzo hii hatimae walio pita ni 15 ambapo wabunifu wa tatu wanatoka nchi za jirani ambazo ni Lubumbashi DRC, Nairobi Kenya na Terni Italy,” amesema Mustapha Hasanali.
Ameongeza kuwa wengine wametoka Tanzania katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Pwani na Dodoma.
Huu ni msimu wa 15 wa tamasha la Swahili Fashion Week ambalo litafanyika kuanzia Desemba 2 mpaka 4 jijini Dar es Salaam.