BAADHI ya wabunge wamezungumzia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wakisema ufisadi unaoendelea nchini ni matokeo ya kupuuzwa kwa ripoti za mkaguzi huyo.
Maoni ya wabunge hao yametolewa baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuibua ufisadi mkubwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Serikali Kuu kwa ukaguzi ulioishia Juni mwaka jana.
Wakizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge jana, wabunge wengi wamesikitishwa na kitendo cha Serikali kufumbia macho ripoti hizo huku wengine wakisema wabadhirifu wote serikalini ni wezi wanaostahili kushtakiwa na kufilisiwa.
Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Baruwani (CUF), alisema kwa mfumo wa sasa ni vigumu ubadhirifu wa fedha za Serikali kukomeshwa kwa vile ni watendaji wanaotakiwa kusimamia ripoti hiyo ndiyo wanaohusika na wizi huo.
“Kesi ya mbuzi huwezi kumpelekea fisi, ninachokiona mimi hapa inabidi CAG apewe meno maana kwa sheria ilivyo CAG akikagua anaishia kutoa ripoti tu baada ya hapo kazi ni ya watu wengine.
“Tumeona udhaifu huo, sisi kama Bunge inabidi tuishauri Serikali ilete sheria tuifanyie mabadiliko CAG aongezewe meno haya mambo yatakwisha,” alisema.
Laizer
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), aliitaka Serikali kufungua macho juu ya ripoti za CAG na kueleza kuwa bila hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watendaji wabadhirifu fedha nyingi zitaendelea kupotea.
“Hawa watendaji wanaoisababishia Serikali hasara inabidi washitakiwe na wafilisiwe. Mgonjwa bila dawa hawezi kupona lakini pia mwizi bila kukamatwa na kuadhibiwa hawezi kuacha kuiba,” alisema.
Alisema inasikitisha kuona kila mwaka mkaguzi huyo anaendelea kufanya ukaguzi na kubaini uchafu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. “Fedha hizi ni sawa na bajeti nzima ya wizara moja lakini zinapotea,” alisema.
Ntukamazina
Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM), alisema ubadhirifu wa aina hiyo hauwezi kumalizika iwapo rais wa nchi hatakua mkali kupambana na ubadhirifu.
Ntukamazina anayejulikana kama senior citizen (raia mkongwe), alisema CAG hawezi kuongezewe meno zaidi ya hapo na kwamba kinachotakiwa ni mamlaka ya nchi kulitambua hilo na kulisimamia.
“Utekelezaji wa ripoti hizi ni suala la leadership (uongozi), huwezi kupambana na ufisadi kama wewe si msafi. Katika hili Serikali inabidi ichukue hatua, tunaposema Serikali ni rais, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuajiri na kuwafukuza hawa watendaji.
“Mchezo huu wa kulindana hatufiki mbali. Mimi siku zote nimekuwa nikikosoa ninapoona Serikali inakosea na baadhi ya mawaziri wamekuwa wakinichukia, lakini nasema rais anatakiwa awe serious (dhamira ya dhati) na hizi ripoti za CAG,” alisema.
Rweikiza
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM), alisema waliohusika na ubadhirifu uliotajwa na CAG ni majambazi kama majambazi wengine.
“Hao ni majambazi tu, ingekuwa ni China watu hao wangepigwa risasi.Kwa mfano mtu anaendelea kulipa fedha kwa watu waliostaafu au kufariki dunia, huo ni ujambazi tu, kimsingi wanapaswa kushitakiwa mara moja,” alisema.
Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila NCCR-(Mageuzi), alisema kila mwaka ripoti za CAG zimekuwa zikianisha madudu lakini hakuna hatua zinazochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
“Nini kifanyike, ripoti hizi inabidi apewe PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) halafu wabainishe kesi za jinai zilizomo nani anahusika na uhalifu gani wawapeleke moja kwa moja mahakamani.
“Shida iliyopo hapa ni mfumo; CAG anakagua anaishia kukagua tu anampa TAKUKURU ambaye naye hana meno halafu anapeleka kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka), zikienda kule kesi nyingi zinakufa,” alisema.
Juzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad alitoa ripoti yake inayoonyesha ubadhirifu mkubwa katika maeneo mbalimbali ikiwamo, mishahara hewa, misamaha ya kodi, usimamizi mbovu wa mipango miji na wastaafu hewa kuendelea kulipwa nje ya nchi.
Ripoti hiyoiliitaja Wizara ya Ujenzi kuwa inaongoza kwa kudaiwa na wakandarasi.
Profesa Assad alisema wizara hiyo inayoongozwa na Dk.John Magufuli inadaiwa Sh bilioni 800.
Ukaguzi huo pia ulibaini kuwa wafanyakazi walioacha kazi au kustaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao, na hadi ripoti hiyo inatolewa Sh milioni 141.4 zimelipwa kwa wafanyakazi hao walioacha kazi.
ZITTO
Naye Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameishauri Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwabana maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waeleze upotevu wa Sh bilioni 836.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2013/14, mizigo iliyobaki nchini kwa udanganyifu ilikuwa zaidi ya bidhaa 6,000 ambazo zilipaswa kulipiwa kodi ya Sh bilioni 836 lakini haikulipwa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema hali si nzuri kwa sababu mapato mengi ya Serikali yameendelea kupotea.
“Wakati haya yanatokea, Serikali inakabiliwa na ukata mkubwa na inashindwa kuendesha miradi mbalimbali. Fedha iliyokwepwa idara ya forodha pekee inalipa madeni yote ya wakandarasi wa barabara wanaoidai TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania).
“Fedha hizi zingelipa madeni yote ya mifuko pensheni inayoidai Serikali,kulipia miradi miwili mikubwa nchini ya BVR na mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambayo inasuasua kutokana na ukata,” alisema Kabwe katika taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, amemtaka CAG kuweka wazi wafanyabiashara wote walioagiza bidhaa zilizobakia nchini na kuingizwa bila kulipa kodi na vyombo vya uchunguzi vichukue hatua za kuwashtaki mara moja.
“Taarifa inaonyesha mizigo inayoingizwa nchini kwenda nchi jirani zinazotumia bandari zetu hubakia nchini na kuingizwa sokoni kitendo kinachosababisha ukwepaji wa kodi,” alisema.
Kuhusu ubadhirifu wa Sh bilioni 163 katika Kitengo cha Maafa kilichoko Ofisi ya Waziri Mkuu, Zitto alisema: “Huu ni kama mrija wenye wastani wa Sh bilioni 32 kuchotwa kwa kisingizio cha chakula cha maafa kwa wananchi.
“Kwa maelezo ya CAG ni kwamba watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wamekula fedha za chakula cha misaada. Maana hakuna uthibitisho kama mahindi yaliyogawanywa na taarifa kutolewa na Wakala wa Akiba ya Chakula (NFRA).
Alisema Kitengo hicho kimekuwa mrija wa wizi wa fedha za umma.
Zitto ameishauri PAC kufanya uchunguzi maalumu kuhusiana na kashfa hiyo na pia amelitaka Bunge kuchukua hatua stahiki dhidi ya Wizara ya Ujenzi.
Ripoti ya CAG, inaonyesha wizara hiyo ilidanganya Bunge katika kupitisha bajeti ya Sh bilioni 252 ambako kati yake Sh bilioni 87, ziliibiwa au matumizi yake hayaeleweka.
Ziito alisema ACT-Wazalendo kinampongeza CAG kwa kuendelea na utaratibu wa sheria wa kukagua hesabu za vyama vya siasa na kuviasa vyama vichukulie ripoti hiyo kama changamoto ya kutoa kwanza kibanzi katika macho yao.
MWIGULU
Alipotafutwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ili kupata maoni yake kuhusu ripoti hiyo ya CAG alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia hadi pale atakapoisoma.
“Ninachokuomba ndugu yangu kwanza ninahitaji kuisoma ripoti yote ili niweze kusema maana kwa sasa nikifanya hivyo nitakuwa sijawatendea haki Watanzania,” alisema Mwigulu