25.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Wabunge waungana kuishukia Nida

Ramadhan Hassan -Dodoma

WABUNGE wameungana bila kujali itikadi zao kutaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), ichukuliwe hatua kwa kutoweza kutoa vitambulisho kwa wakati.

Walisema hayo walipokuwa wakichangia  mjadala wa taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2018/19.

Mbunge wa Jang’ombe, Ally Hassan King (CCM), alisema Nida inatakiwa kubeba msalama wa watu waliosajili laini za simu za watu wengine kutokana na kushindwa kuandikisha watu kwa wakati huku akidai hata yeye hana kitambulisho cha Taifa.   

“Nije katika suala la vitambulisho hata mimi sina kitambulisho cha Taifa, nilianza kujiandikisha mwaka 2014 tumeandikisha kila mwaka unapigwa danadana. Watu wamesajiliana (laini za simu) kupitia vitambulisho hili kosa ni la nani? Hili kosa ni la Mamlaka  ya Vitambulisho,”alisema.

Mbunge wa Nachingwea, Hassan Massala (CCM)  alitaka watumishi wa Nida wachukuliwe hatua kutokana na uzembe walioufanya ambapo watu wengi hadi sasa hawana Vitambulisho vya Taifa.  

“Nida baadhi ya maeneo kuna uzembe, tungechukua hatua kwa uongozi wa Nida leo nipo hapa napokea simu wananchi hawana vitambulisho, ukienda kwa watu wa Nida hawana mashine za kufanyia kazi kuna watu wamepewa dhamana wanashindwa kusimamia jambo hili halivumiliki, wametuingiza sana katika hasara Nida,”alisema.

Mbunge wa Bunda, Mwita Getere (CCM) alisema fedha za Nida zimetumika vibaya huku watu wakiendelea kuteseka kwa kukosa vitambulisho.

“Nida zimetumika vibaya watu hawana vitambulisho utakuta watu wapo kila siku tunaletewa yale yale hoja hiyo hiyo ifike wakati tutengeneze utaratibu tuamue wenyewe,”alisema Getere.

Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema) alisema kuna ubadhilifu wa kutisha Nida huku wengi wakiwa hawana vitambulisho hivyo alihoji ni kwanini walinunua mtambo ambao  hauendani na ule uliopo. 

“Kwenye ripoti ya CAG wameweka dosari kuu mtambo wa malighafi ni hafifu zimeletewa mtambo ambao haendani mheshimiwa Spika wote tunajua Watanzania wanapata matatizo sababu ya kutokuwa na vitambulisho,kuna mapato mengi yanapotea sana,”alisema. 

Mbunge wa Maswa, Beniventura Kiswaga (CCM) alisema kuna upungufu makubwa  Nida ambapo imefika wakati wananchi wanasafiri kutoka eneo mojakwenda makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kupiga picha.

“Tumeona upungufu Nida, Nida wananchi wanashida kubwa imefika mahali wananchi wanaambiwa wakapige picha makao makuu ya wilaya, kuna vifaa havijatunzwa vizuri hao waliopaswa kuvitunza hawajachukuliwa hatua,”alisema.

 “Tumeona fedha ambazo zinapotea kwenye mashirika ni nyingi sana na yanatumia fedha nje ya bajeti wakati yana muda wa kupanga bajeti  hili haiingia akilini hata kidogo

“Kuna tatizo la kutokuchukua hatua pale kunapokuwa kuna mapungufu kwani haiwezekani kila mwaka Shirika ni hilo hilo. Sisi kama Bunge sasa ni kama tunapoteza muda niombe sana ni vizuri yafanyiwe kazi kwa muda,”alisema.

Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) alisema Serikali inadaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) zaidi ya Sh bilioni 101, Serikali inatakiwa kuzilipa ili dawa ziweze kufika  maeneo mengi.

“MSD wamekosa zaidi ya  bilioni 101 hizi fedha kwa sababu Serikali inadaiwa. Tunataka Waziri wa Fedha na Mipango  atuambie ni kwanini haitaki kulipa deni hili kuna shida sana Serikali kutokulipa madeni.

Pia alisema  mifuko ya hifadhi ya jamii,  inadaiwa zaidi ya Sh trilioni 2,alitegemea  Serikali italipa deni hilo ili wastaafu waweze kupata fedha zao kwa wakati.

“Tulitegemea Serikali ingekuwa imelipa lakini kwa mwaka huu deni limeongezeka, wakati tunaunganisha tulisema tunapunguza matumuzi ya fedha na kuongeza ufanisi, kinachoonekana hali imekuwa mbaya na Serikali inazidi  kukopa sasa itashindwa kulipa fedha kwa wastaafu, wastaafu wamelitumikia kwa muda mrefu Waziri wa Fedha na Mipango,  atumbie fedha hizi zitalipwa lini? Alihoji Mwakajoka.

Kuhusu Shirika la Usafiri Dar es salaam (Uda)  na Wakala wa Undeshaji  wa Mradi wa Mwendokasi (Udat), Mwakajoka alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kuhusu ubadhilifu uliojitokeza ambapo pia alidai Ofisi ya CAG imeuona ubadhilifu huo.

“Nakumbuka mwaka 2013, Shirika la Uda lilingia mkataba na Simon Group .Tunataka kujua Serikali inachukua hatua gani kuhusiana na hisa zilizotolewa, Serikali ina kigugumizi gani kwani CAG ametoa ushauri lakini Serikali inasita kwanini inasita.Watu wamefisadi fedha za umma wapo tu mtaani,”alisema Mwakajoka.

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) alisema  baadhi ya mawaziri wasichukulie uzalendo wa rais kuiumiza nchi ambapo alihoji Sh bilioni 1.5 zilizotumiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii zimeenda wapi.

“Wezi bado wapo angalieni wapi wafanyabiashara wanaiba fedha za umma, kwanza ni kwenye bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi hapa ndipo nchi inaibiwa, haya nimeyaona sana watu wanaangiza bidhaa wanauza ndani ya nchi.

“Sehemu nyingine ni bidhaa zilizoagizwa na kupatikana kuwa na makosa katika forodha, hapa watu wanapiga pesa bidhaa zilizoagizwa kwa kuuzwa nje ya nchi lakini zikabaki hapa nchini.

“Natoa ushauri TRA pamoja na kazi nzuri inayofanywa waanzishe kitengo cha kuangalia miamala yote, tukiacha tutaendelea kupigwa,”alisema Kingu.

Majibu ya mawaziri

Kuhusu malighafi za kutengenezea vitambulisho, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene,  alisema lengo lilikuwa ni kutengeneza vitambulisho milioni 24 lakini hadi sasa vitambulisho milioni  sita ndo vimetengenezwa.

“Tulitaka kuchezewa tu kwamba mashine mpya haziwezi kutumia kadi mpya, waliotuuliza masine mpya ilikuwa waje sasa lakini wamechelewa sababu ya corona

“Mashine hizi kwa saa moja inazalisha vitambulisho 4,500, saa  mbili vitambulisho 9,000 masaa 16 sawa na siku moja vitambulisho 144,000,” alisema Simbachawene.

Ahitimisha kwa hoja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema Sh bilioni 1.5 ambazo wabunge wamehoji matumizi yake, alisema zilitumika kutangaza utalii na faida yake itakujakuonekana baada ya miaka mitatu au mitano.

“Mwanzo kulikuwa kuna bilioni 5.4  lakini tulipunguza na waziri alikuwa anaumwa, tulipunguza hadi ikafika bilioni 1.5 ,watu wanahoji kuhusu wasanii ili tuvute watalii nilazima tuwalipe wasanii,” alisema.

Wakati akiendelea kuchangia Mbunge wa Viti Maalum Lucy Mollel (Chadema) alimpa taarifa kwamba suala linalohojiwa na wabunge si wasanii bali ni fedha kutumika nje ya bajeti.

Akiendelea kuchangia Hasunga alisema “hoja ilikuwa nje ya bajeti, ni kwamba bajeti ilikuwa haitoshi kulikuwa na mfuko wa fedha wa  kuendeleza utalii ndio zilichukuliwa kutangaza utalii.

 “Taasisi ya uhifadhi zina fedha kwa ajili ya kupromote utalii lakini tarehe 16 mwaka 2019 waliandika barua ambayo baada ya kuona zile fedha hazikuwa katika bajeti waliomba hazina kwa ajili ya matumizi ya fedha hizo.

“Huwezi kutangaza utalii leo ukaona faida leo, hii ni investment majibu na faida  tutapata baada ya miaka mitatu au mitano, natakakusema matumizi haya faida yake yataonekana kadri tunavyoenda,”alisema.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango, akijibu hoja ya wabunge juu ya Benki Kuu (BoT) na fedha chakavu alisema kuhesabu fedha zilizochakaa zinachukua muda mrefu hivyo zoezi hilo limekuwa likichukua muda mrefu.

Alisema katika kukabiliana na jambo hilo, Serikali ilinunua mashine 10 kwa ajili ya kuhesabu fedha zilizochakaa.

“Kuhesabu fedha kwa mkono inachukua muda mrefu, tumefanya mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupokea zile ambazo ni safi na kuendelea kutoa elimu ili hizi fedha zisichakae mapema,”alisema

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, akijibu baadhi ya hoja za wabunge alisema wamejipanga kushughulikia matatizo yaliyopo Mamlaka ya Bandari Tanzania  (TPA) , ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria ya manunuzi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,567FollowersFollow
517,000SubscribersSubscribe

Latest Articles