25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wataka bajeti iguse wananchi

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

WAKATI bajeti kuu ya Serikali ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, wabunge wameeleza matarajio yao, huku wengi wakisema wanatarajia itagusa wananchi na fedha zinazokusanywa na Serikali Kuu zitashushwa katika halmashauri.

CHEGENI 

Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema makusanyo yanayokusanywa na Serikali yanatakiwa kuendana na fedha kwenda kwa wananchi.

“Hela yote inakuja Serikali Kuu, inatakiwa makusanyo yaendane na matumizi, lakini ni lazima tumshukuru Rais, kwa sasa watu wanafanya kazi na hakuna kubweteka,” alisema.

MARWA 

Mbunge wa Viti Maalumu, Agnes Marwa (CCM), alisema bajeti ya leo ni lazima iangalie suala la Serikali kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

“Ndoa nyingi zinavunjika sababu ya kukosekana kwa maji, matokeo yake kunakuwa na ongezeko la  watoto wa mitaani,” alisema.

GULAMALI 

Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali (CCM), alisema matarajio yake ni kuona bajeti ya Serikali imejikita katika mambo yanayowagusa wananchi moja kwa moja.

“Matarajio yangu ni kuona bajeti ya Serikali imejikita katika mambo yanayowagusa moja kwa moja wananchi, ujenzi wa miundombinu na maji,” alisema.

Alisema pia bado kuna uhitaji wa kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi, hivyo anatumaini Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kufufua umeme wa Rufiji.

KABOYOKA 

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, alisema bajeti hiyo  haitamsaidia mwananchi wa kipato cha chini. 

Kaboyoka ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), alisema anaamini bajeti ya mwaka huu haitamsaidia mwananchi wa chini kwani kuna baadhi ya maeneo hayajapewa fedha za kutosha.

Alisema hakuna jambo linalomuumiza kama jinsi ambavyo wananchi wametumia nguvu kujenga shule na zahanati, huku Serikali ikishindwa kuzimalizia.

“Maboma mengi wamejenga wananchi, lakini Serikali haitengi fedha kwa ajili ya kumalizia maboma hayo, sijafurahi kabisa na bajeti kama haitaonesha hayo,” alisema.

Kaboyoka pia alisema Tanzania imekuwa ikipata watalii wengi, lakini akahoji ni kwanini Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) imekuwa ikipewa mzigo mkubwa bila ya kupewa fedha.

“Tanapa ni kama wanalipa kodi mara mbili, inalipa kodi zaidi ya asilimia 30 kwenye mapato hasi, Mungu katupa nafasi hii ya kuwa na wanyama, tuboreshe, tuwaache wafanye kazi,” alisema Kaboyoka.

Aidha, aliitaka Serikali kuiangalia Bohari ya Dawa (MSD) kwani imekuwa na madeni makubwa wakati Serikali ikidai imetenga fedha za kutosha kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

“Kwanini wizara inaonesha kuna fedha wakati MSD kuna madeni makubwa, kamati yangu ilifika kule, kule kuna shida, sasa hivi MSD imepata nafasi ya kusambaza dawa Afrika Mashariki wakati hapa nyumbani inashindwa, tuisaidie,” alisema.

MWAMBE 

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema), alisema bajeti ya leo sio halisi kwani iliyopita imetekelezwa chini ya asilimia 60 tu.

Alisema miradi mingi inagusa maisha ya vitu na sio watu, hivyo Serikali inatakiwa iliangalie hilo.

“Bunge linaidhinisha fedha, lakini Serikali haipeleki, miradi mingi haitekelezwi, hasa ile inayogusa watu, miradi mingi inagusa vitu, hivyo bajeti imekuwa kama ‘fashion’ tu, haitekelezwi,” alisema Mwambe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles