23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAPITISHA BAJETI YA ARDHI, MBOWE AMSIFU LUKUVI

MAREGESI PAUL NA RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

WABUNGE wamepitisha Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2017/18, huku Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi, akizitaka  Halmashauri zote zisiruhusu watu kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa.

Pia wabunge wa upinzani, wakiongozwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, walimsifia na kumpongeza Lukuvi na watendaji wake kwa kutatua kero za ardhi.

Aidha, wabunge hao, wameitaka serikali kuanza kuweka mikakati rasmi na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kupima na kukagua ardhi yote nchini na kuipangia matumizi, ili kuepusha Watanzania kuingia katika vita kwa sababu ya migogoro ya ardhi.

Akichangia katika majadiliano ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mbowe alimpongeza Lukuvi na Naibu Waziri wake, Angelina Mabula, kwa kazi wanayoifanya kwenye wizara hiyo bila kuangalia itikadi za kisiasa.

“Naomba nisiwe mchawi, nami niseme hili, nakupongeza sana Waziri na Naibu wako kwa kazi nzuri mnayofanya kwenye wizara hii, sifa hizi tunazowapa naomba mzitendee haki kwa kuendelea kuwajibika, lakini pia mawaziri wengine sasa waige mfano wenu,” alisema Mbowe.

 Pia Mbowe aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha inafanya ukaguzi wa ardhi mkoani Kilimanjaro, kwa kuwa kwa sasa mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa ardhi, wakati kuna ongezeko kubwa la watu.

 “Naomba mfanye ‘auditing’ ya ardhi katika mkoa ule, watu wamejenga hovyo, siku hizi Moshi kuna makazi holela, watu wanajenga hovyo hakuna hata sehemu ya kupitishia feeder roads,” alisema.

Aidha, Mbowe aliitaka wizara hiyo kuyafanyia tathmini mashamba makubwa yaliyopo mkoani Kilimanjaro yaliyotaifishwa kutoka mikononi mwa wakoloni kipindi cha enzi za Mwalimu Nyerere, ambayo kwa sasa yanashikiliwa na watu wachache.

 

CHIKOTA

Kwa upande wake, Mbunge wa Nanyama, Abdallah Chikota (CCM), alisema kutokana na uongozi wa wizara hiyo ya ardhi kuwajibika ipasavyo, kwa sasa kuna mabadiliko makubwa tofauti na zamani, hasa katika huduma.

“Wizara imepunguza watu wengi kurundikana wizarani, imepeleka shughuli zake kikanda,” alisema.

Alisema kwa kazi aliyoifanya Lukuvi ya kutembelea maeneo mengi yenye migogoro, tatizo la mgogoro ya ardhi linaanza kuwa na ahueni ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

“Awamu ya tano mmejitahidi sana, migogoro ya ardhi imepungua, bado kuna kazi kubwa, ila bado kuna kazi kubwa ya kulipatia ufumbuzi tatizo hili, lazima ifike mahali tuipangie matumizi ardhi yetu, wakulima na wafugaji wawe na maeneo yao bila kuingiliana,” alisema.

 

ISHENGOMA

 

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Christian Ishengoma (CCM), alisema katika maeneo yote yenye migogoro ya ardhi, mkoa huo unaongoza kutokana na kuwapo kwa matukio ya mapigano na wakati mwingine hadi kuuana baina ya wafugaji na wakulima.

Dk. Ishengoma aliipongeza wizara hiyo  kutokana na jitihada zake za kutafutia ufumbuzi migogoro hiyo, huku akidai vurugu baina ya wafugaji na wakulima kwa sasa zimepungua.

“Ila mie naamini dawa ya hii migogoro kwa kweli ni kupima, kukagua na kuipangia ardhi yetu matumizi. Kwa hapa Morogoro Wizara hii ya ardhi imefanya vizuri, kwani maeneo mengi tu yameanza kupimwa,” alisema.

 

MDEE

 

Kwa upande wake, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alitumia muda wake kumpongeza pia Waziri Lukuvi kwa kazi yake nzuri anayoendelea kuifanya kupitia wizara hiyo, ikiwamo jitihada zake za kumaliza migogoro ya ardhi.

Alimtaka waziri huyo kuendelea na uwajibikaji wake, lakini pia katika kudhibiti watu wanaojirundikia viwanja vikubwa bila kuviendeleza, awachukulie hatua kwa mujibu wa sheria bila kujali itikadi zao, majina yao makubwa wala nafasi zao.

 “Naomba kusiwe na double standard katika hili, kama kuna kada wa CCM au Chadema chukua hatua. Usipokuchukua hatua tutakusulubu kwa double standard,” alisema.

 Kuhusiana na mgogoro wa muda mrefu wa viwanja 20,000, aliomba wizara hiyo ifanye ukaguzi kwa viwanja hivyo, kwani vingi vimegeuzwa maslahi ya wajanja wachache.

 

MAKILAGI

 

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi (CCM), alisema bado Tanzania ina migogoro mikubwa ya ardhi baina ya hifadhi, wafugaji na wakulima, jambo linalohitaji kuchukuliwa hatua za haraka.

“Ifike wakati Serikali ipime ardhi yote ya Tanzania. Suala hili lisiachiwe halmashauri hazina fedha, Serikali itengeneze mkakati maalumu wa kutafuta fedha hata kama ni mkopo kila sekta itengewe ardhi yake, tuishi kwa amani na utulivu,” alisema.

Alisema idadi ya watu imeongezeka, mifugo imeongezeka na matumizi ya ardhi kwa ajili ya kilimo na hifadhi yameongezeka, hivyo ni wakati mwafaka sasa wa kuweka mipango ya namna ya kuitumia ardhi iliyopo ambayo bado ni kubwa.

 

 NASSARI

Naye Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), aliwataka mawaziri wengine katika serikali ya awamu ya tano, kuhakikisha wanaiga utendaji wa Lukuvi, ili kuweza kuifikisha nchi inapotakiwa.

Nassari alisema kiongozi huyo kwa kipindi kifupi amefanikiwa kufanya mambo mengi yaliyokuwa yanaisumbua wizara hiyo.

 

 UMBULA

 

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Umbulla (CCM), alisema jambo linalotakiwa kufanywa kwa sasa ni kumaliza migogoro ya nchi pamoja na kubuni mipango madhubuti na kuhakikisha Watanzania wanaishi katika nchi yao bila kuwa na migogoro ya ardhi.

“Kubwa ninaloliona ni kubadilisha mindset, nashauri serikali tutumie rasilimali zetu tulizonazo tuweke mipango bora ya matumizi yetu ili kuondoa kero za wakulima na wafugaji, tusipojiandaa sasa hivi kuna hatari vizazi vijavyo vikaishia kupigania ardhi yao,” alisema.

 

 MABULA

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Angelina Mabula, alisema Wizara hiyo itaendelea kutatua migogoro ya ardhi.

Alisema kuhusiana na bei kubwa za nyumba za Nation Housing, kinachochangia ni gharama za barabara, huduma za maji, huku akidai Rais alishalitolea ufafanuzi jambo hilo.

“Hapa gharama zinakuwa kubwa sababu ya mradi kugharamikia kila kitu, mfano maji, barabara, lakini Rais alishatolea ufafanuzi juu ya jambo hilo,” alisema.

 

LUKUVI AJIBU

 

Akifanya majumuisho ya michango ya wabunge waliochangia, Waziri Lukuvi alisema Wizara hiyo itaendelea kutekeleza mwongozo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, wa kutenda haki kwa Watanzania wote bila  kuangalia itikadi ya vyama.

“Hakuna jambo ambalo sikuandika, ingawa sikuandika yote naweza kusema tulikuwa  ‘serious’ katika kujadili mjadala huu, sisi kama Wizara tutaendelea kutekeleza mwongozo wa Rais, yeye ni Rais wa CCM,  amekuwa akisisitiza tutoe huduma bila ubaguzi wa aina yoyote.

Tuendelee kushirikiana, moto ni huo huo, hapa nyuma yangu nimeleta viongozi wote wa Kanda nane, hivyo kila jambo mlilosema kama linahusu mambo ya ardhi msajili yupo, kama Kanda ya Magharibi Kamishna na Msajili wapo,” alisema.

Alisema moja ya mambo waliyoyajadili wabunge wengi ni kukwama kupimwa mashamba kwa sababu ya ukosefu wa vifaa, alidai kwa sasa vifaa vimeshafika na vitawafikia muda si mrefu.

“Tumeshaagiza vifaa na tumetangaza katika magazeti tutavisambaza tena kwa teknolojia mpya kwa sababu sasa tunatumia ‘satelite’ na vifaa vya mapokezi ya satellite, tumewaonesha sasa tutakuwa na vifaa vipya na tutawaelekeza maofisa wenu, kwani hawajui jinsi ya kuvitumia.

“Wilaya yako yote inaweza kupimwa kwa siku tano au sita, tumeagiza na tutasambaza katika kanda na awamu ya pili tunataka tusambaze katika kila wilaya, hata kama unamwita mpimaji binafsi inapunguza gharama,” alisema.

Lukuvi alisema kwa sasa wanateua watendaji katika kanda ili waweze kufanya kazi hiyo, huku akidai matatizo yote ya Dar es Salaam na Dodoma watayamaliza ndani ya muda mfupi.

“Inawezekana mkirudi baada ya muda mtakuta yamekwisha kwa sababu watendaji wangu wote wa kanda wapo hapa wamesikiliza na sasa tumewawezesha na magari wanakimbia kila mahali na tutakuja huko mkoani tutajadiliana sana juu ya changamoto zilizopo.”

Alisema kazi ya kubatilisha mashamba ambayo hayatumiki pamoja na kukagua mashamba yasiyotumika wataianza mara moja, huku akidai pia lengo lao ni kupima kwa kasi viwanja ili kila mmoja aweze kumiliki kiwanja.

“Ingawa bado mnazungumza gharama, lakini hizo gharama tumepunguza tozo kwa asilimia 67, hata nyie wabunge mna ofa niliyowapa mimi angalieni ile kitu inaitwa ‘Premium’, asilimia  67 imepungua umilikishaji utakuwa nafuu sana.’’

Waziri Lukuvi alizitaka Halmashauri zote zisiruhusu watu kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa, ili kupunguza migogoro ya ardhi inayoweza kutokea.

“Kwa sababu kilio chao cha kupunguza tozo tumefanya na gharama za upimaji zitapungua sana na hivyo hakuna sababu ya mtu kuendelea kuvamia vamia pamoja na kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa,’’ alisema.

Kuhusiana na hoja ya ukosefu wa watumishi, Waziri Lukuvi alisema watashirikiana na Tamisemi ili kulitatua tatizo hilo.

Alisema katika zungukazunguka yake amegundua kuna wilaya zimependelewa kwa kupangiwa watumishi wengi, huku akizitaja Wilaya za Ilemela na Nyamagana kuwa zimepangiwa watumishi zaidi ya 100.

“Katika zungukazunguka yangu nimegundua kuna wilaya zimependelewa kwa kupangiwa watumishi wengi sana, Ilemela na Nyamagana wana watumishi wasiopungua 100 wilaya mbili kwa sekta ya ardhi.’’

Alisema watawaondoa wafanyakazi hao na kuwapangia maeneo mengine kwa sababu kuna wilaya ambazo hazina watumishi wa ardhi hata mmoja.

Alisema kabla ya kuajiri wafanyakazi wapya katika sekta ya ardhi, wataangalia uwiano wa wale walioajiriwa jinsi walivyopangwa ili wawekwe vizuri na kazi za dharura ziweze kufanyika.

“Tutaangalia uwiano wa jinsi walivyopangwa ili kazi za dharura ziweze kufanywa kwa watumishi waliopo ili waweze kusambazwa maeneo mengine, watu watapangwa upya halafu baada ya hapo tutasimamia vibali kwa Mheshimiwa Kairuki, kwani upangaji haukuwa mzuri tutaurekebisha.

“Masuala haya ya upangaji na kodi ya asilimia 30 kinachosisitizwa hapa tungependa miji yetu ipangwe watu wajenge kwenye viwanja vilivyopangwa, lakini watu wamilikishwe mashamba angalau wapate hati,’’ alisema.

Alisema kuhusiana na kutoza kodi kwa mashamba ya mji na vijijini, Serikali itasimamia ili mashamba hayo yapimwe ili waweze kupata fedha.

 

mwisho

……………

Tanesco yajipanga kuukwamua mradi wa umeme Dar

Na ASHA BANI

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), wamekubaliana kuanza  mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa Kilovolti 132 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mradi huo ulikwama kuendelea utekelezaji wake katika eneo la Barabara ya Mandela, Ubungo hadi Kurasini, kutokana na Tanroads kutaka kuanza mradi wa ujenzi wa barabara sita katika eneo moja na kunakotakiwa kupita mradi wa umeme.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika eneo litakalopita mradi huo Ubungo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Juliana Pallangyo, alisema mazungumzo yamefikia pazuri na kwamba mradi huo unatarajiwa kumalizika Agosti, mwaka huu.

Alisema awali kulikuwa na Kilovolt 33 na kwamba kutokana na umuhimu wa kukuza njia hiyo, wanaongeza hadi 132 na kueleza kuwa tatizo la umeme Mkoa wa Dar es Salaam, litakuwa limekwisha.

Aliendelea kueleza kuwa, Tanesco na Tanroads wanajenga nyumba moja na vyote vinavyoendelea kufanyika ni kwa manufaa ya serikali na wananchi, hivyo ni lazima mradi huo uwekwe ili kuwaondolea adha ya umeme wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Naye Meneja Mwandamizi wa mradi huo kutoka Tanesco, Gregory Chegere, alisema lengo ni kuboresha umeme Dar es Salaam na kama mradi ukikamilisha shida za kukatika katika kwa umeme zitakuwa zimekwisha.

“Mradi huu ukikamilika utasaidia endapo umeme ukikatika sehemu moja, mfano Ubungo, basi Kurasini watakuwa na uwezo wa kuwagawia wa Ubungo na wakaendelea na kushughuli zao kama kawaida,” alisema Chegere.

Alisema mradi huo wa njia ya usafirishaji wa umeme unaosimamiwa na Kampuni ya SAE Power Lines, utagharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 32.25, ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia.

Alieleza licha ya kuwa na mafanikio, lakini wamepata changamoto wakati wa hatua ya ubunifu ‘designing stage’ na ndilo ambalo limechelewesha kukamilika kwake.

Alisema mradi huo utaendelea katika mikoa mingine, ikiwa ni pamoja na Kilimanjaro na Arusha, baada ya kukamilika kwa Dar es Salaam.

Kwa upande wa Tanroads, Injinia Eliseus Mtenga alisema tatizo lililotokea wakati Tanesco wanapanga kuendelea na mradi huo na wao walipata ufadhili wa Benki ya Dunia kupanua barabara kuweka njia sita katika eneo hilo hilo.

Alisema walitakiwa kutanua barabara na kuacha mita kumi kutoka njia ndogo ‘service roads’, lakini wanakwenda kuyazungumza na kuamini watakaa sawa na kuelewana nini kifanyike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles