Na Khamis Mkotya, Dodoma
BAADHI ya wabunge wamekosoa mchakato wa ugawaji wa majimbo ya uchaguzi huku baadhi yao wakisema Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), imekurupuka katika jambo hilo.
Wakizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge jana, wabunge hao walisema hawaoni sababu za tume kugawa majimbo katika kipindi hiki ikizingatiwa umebaki muda mfupi uchaguzi ufanyike.
Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), alisema lengo la kugawa majimbo ni jambo jema, lakini tatizo ni muda na kwamba hizo ni hila za CCM za kutaka kujiongezea majimbo.
“Kwa kweli Tume ya Uchaguzi wamekurupuka kutangaza mchakato wa kugawa majimbo. Unagawa majimbo leo wakati imebaki miezi miwili nchi kuingia katika kampeni?
“Utafiti wamefanya lini, hili ndilo suala… leo baadhi ya wabunge wa Zanzibar wanalalamika kwamba katika mchakato huo majimbo yao yamefutwa katika dakika za mwisho,” alisema.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema dhamira ya Serikali katika jambo hilo ni nzuri lakini tatizo ni Tume ya Uchaguzi.
“Huu si muda wa kugawa majimbo, nia ni nzuri lakini wangefanya mapema. Kesho uchaguzi leo unawaambia watu kuwa majimbo yanagawanywa kwa kweli katika hili tume wamekurupuka,” alisema.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), aliishangaa tume hiyo kutangaza mchakato wa kugawa majimbo wakati muda uliopo ni mfupi kabla ya uchaguzi.
“Mtu yeyote mwenye mtazamo pevu hawezi kuwaelewa Tume ya Uchaguzi, bado siku 50 kampeni za uchaguzi zianze mnatangaza kugawa majimbo utafiti wenu mlifanya lini?” alisema.
Naye Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alisema katika jambo hili ni wazi kuwa NEC haikujiandaa na kusema kuwa huko ni kuiongezea mzigo Serikali.
“Tume hawakujiandaa, unagawaje majimbo leo na uchaguzi ni kesho? Huo mchakato utafanyika kwa namna ipi bila kufanya utafiti, serikali inakuwa na mambo mengi ya kufanya katika kipindi kifupi.
“Hivi sasa wananchi wengine wamekwisha kuandikishwa katika daftari la wapiga kura wanajua na mbunge watakayemchagua ni yupi, leo unawaambia jimbo limefutwa au limegawanywa haileti maana. Ni vema mambo haya wangefanya mapema,” alisema.
Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM), alisema anachofahamu yeye ni kwamba tume ilianza mchakato huo mapema lakini tatizo lililopo ni usiri katika jambo hilo.
Juzi, NEC ilitangaza kuanzisha mchakato wa ugawaji wa majimbo kuanzia leo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa wabunge utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Damian Lubuva majimbo hayo yanagawanywa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 75 (3) na (4).
Jana NEC kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Kombwey, ilisema majimbo mapya yatakayogawanywa yatatangazwa ifikapo mwishoni wa Juni mwaka huu.