NA HAMISA MAGANGA, DAR ES SALAAM
UWEZO mdogo wa baadhi ya wabunge kuchambua bajeti kwa kina unachangia kupitishwa bajeti mbaya ya Serikali kila mwaka.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali inayohusika na masuala ya afya (Sikika), Irene Kiria, wakati wa majadiliano ya namna ya kuboresha uandaaji na upatikanaji wa bajeti nzuri ya Serikali.
Alisema wabunge wanapaswa kuongezewa uwezo wa kuchambua bajeti ipasavyo ili kuepuka kupitisha mambo ambayo hayana ulazima.
“Bunge linatimiza wajibu wake kukosoa na kupitisha bajeti za wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, nadhani linahitaji kuimarisha uwezo wake wa kuchambua bajeti kwa kina na kuirekebisha kabla ya kuipitisha.
“Ili lifanikiwe katika hilo, kamati zake zote zinatakiwa zipitie na kuchambua MTEF (Medium Term Expenditure Framework) na si vitabu vikuu vya bajeti pekee (memorandum),” alisema Kiria.
Alisema MTEF ndiyo kitabu mama cha bajeti ya Serikali, kinachoainisha matumizi kwa kina na vitabu vikuu vinavyotumiwa na wabunge kwa ajili ya kuidhinisha, japo havionyeshi matatizo yanayohitaji ufumbuzi.
Kiria alisema ili wadau mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara, wanahabari, wakulima, taasisi huru na wananchi wote waweze kuchambua na kutoa maoni yao kuhusu mwelekeo wa bajeti, ni muhimu vitabu, hasa MTEF za kila wizara ziwekwe wazi mapema.
“Bajeti ya Serikali inatakiwa kutekeleza malengo mahususi, imekuwa ikifanyika hivyo, kuna maeneo machache ambapo shughuli zinazopangwa kutekelezwa hazifikii malengo yaliyopangwa.
“Serikali inapaswa kudhibiti maeneo ambayo hayana tija, mwisho wa siku utakuta inarudia matatizo yaleyale,” alisema.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo hayana umuhimu na hupangiwa bajeti kubwa kuwa ni kulipa posho, mafunzo, safari, viburudisho, ununuzi wa magari, mafuta na vilainishi.
Alisema maeneo hayo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo yalipangiwa Sh. bilioni 626.3 (2011/2012), Sh. bilioni 681.2 (2012/2013) na Sh. bilioni 714.1 mwaka wa fedha 2013/2014.
Kiria alisema angalizo la Sikika linalenga kutoa tahadhari kwa watendaji wanaohusika na kutengeneza bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, kuepuka na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.