30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge walioshitakiwa kwa rushwa waachiwa

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

WABUNGE watatu wa CCM waliokuwa wakituhumiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 30 wameachiwa huru.

Hatua hiyo ilifikiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage.

Walioachiwa huru ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54), Mbunge wa Mvomero, Ahmad Saddiq (53) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63).

Hakimu alichukua hatua hiyo  baada ya Mawakili wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa na Emmanuel Jacob kuomba mahakama ifanye hivyo.

“Mheshimia hakimu ingawa kesi imekuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP) amewasilisha hati kuonyesha kwamba hana nia ya kuendelea na shauri hili.

“DPP amewasilisha hati hiyo ya kuomba shauri lifutwe kupitia kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002,” alisema.

Wakili wa washtakiwa hao, Mpale Mpoki, aliiomba mahakama kumpa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo.

Hata hivyo, Hakimu Mwijage alisema shauri linaondolewa kama ambavyo DPP ameomba na washtakiwa wanaachiwa huru.

Hakimu alimuelekeza Wakili Mpoki kupeleka maombi yake katika ofisi za DPP kwa sababu mahakama haiwezi kutoa amri anayoomba kutokana na hatua   hiyo ilipofikia.

Akizungumza baada ya kuachiwa huru, Kangi alidai tangu walipofikishwa mahakamani moyoni mwao walianza na Mungu na wanamaliza na Mungu.

“Leo Mungu katoa majibu tuko huru, hii kesi tulijua tangu mwanzo ilikuwa ya kutunga kwa sababu za siasa.  Takukuru hawakuwa na ushahidi ndiyo maana walikuwa vinyonga na vigeugeu.

“Tutakaa na wanasheria wetu kutafakari tujue nini tunafanya kutokana na udhalilishaji tuiliofanyiwa,”alisema.

Awali, akisoma mashtaka, wakili Jacob alidai   washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kujihusisha na rushwa.

Alidai Machi 15 mwaka huu, kati ya saa 2.00 na saa 4.00 usiku katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wabunge na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta.

Inadaiwa wabunge hao waliomba kiasi hicho cha fedha  kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles