25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAIOMBEA RUZUKU HOSPITALI YA BUGANDO

Na CLARA MATIMO

-MWANZA

WABUNGE wa Kanda ya Ziwa wameiomba Serikali kutoa ruzuku kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), ili isaidie kuboresha huduma za ubingwa kwa wagonjwa hasa wa saratani.

Wakizungumza juzi kwa nyakati tofauti hospitalini hapo wakati wa uzinduzi wa jengo la huduma za matibabu ya Bima ya Afya, wabunge hao walisema ruzuku hiyo itaisaidia BMC kujiendesha hivyo kuwapunguzia wagonjwa wanaotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa adha ya kufuata huduma za mionzi katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), alisema wao kama wabunge wa Kanda ya Ziwa wataipigania BMC ili ipate ruzuku kutoka serikalini itakayoisaidia kuboresha huduma zake iweze kutoa huduma za kiwango cha juu kama zinazotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM), alisema: “Mwaka jana nimewasaidia gharama za nauli  wagonjwa 10 wa saratani toka  kwenye jimbo langu ambao walipewa rufaa hapa BMC kwenda kupata  matibabu ya mionzi Hospitali ya  Ocean Road iliyopo  jijini Dar es Salaam, hivyo endapo Serikali itatoa ruzuku itawasaidia wananchi wa Kanda ya Ziwa ambao wengi wao wanasumbuliwa na ugonjwa huo,” alisema.

Naye Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula (CCM), alisema ni wajibu wa wabunge wa Kanda ya Ziwa kuwasemea wananchi waliowachagua ili huduma zote za kibingwa ziboreshwe na kupatikana BMC maana ukanda huo unao wakazi wapatao milioni 15.

“Naamini Serikali yetu ni sikivu, hasa Rais John Magufuli ambaye nia yake ni kuhakikisha anaboresha huduma za afya kwa wananchi atasikia kilio chetu, tutapewa ruzuku ambayo itatusaidia kuboresha huduma zote hapa BMC ili wananchi wetu wasihangaike  tena kwenda Ocean Road,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Saratani wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), Dk. Nestory Masalu, alisema idadi ya wagonjwa waliogundulika na ugonjwa wa saratani imeongezeka kutoka 3,400 mwaka 2009 hadi 10,200  kwa Desemba mwaka jana, ongezeko hilo limechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli za migodi na asilimia 60 ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu Hospitali ya Ocean Road wanatoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Hapa BMC tumeanza kutoa huduma za mionzi yapata wiki mbili sasa, lakini changamoto kubwa tuliyonayo ni upungufu wa mashine za kutolea huduma hiyo moja, gharama ya kufunga mashine moja ni  Sh bilioni 1. 5, hivyo  endapo tukipata  ruzuku kutoka serikalini kama inavyopewa Hospitali ya Ocean Road, tutaboresha huduma  na kuongeza vifaa tiba  hakutakuwa na mgonjwa atakayeandikiwa rufaa ya kwenda Ocean Road,” alisema Dk. Masalu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika hospitali za wilaya na mikoa yote ya kanda ya ziwa ili kupunguza ongezeko la wagonjwa wanaofika BMC bila kuandikiwa rufaa wakiamini  kuna huduma bora zaidi.

Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh milioni 959,  kati ya hizo Sh milioni 700 ni mkopo ambao BMC ilichukua kutoka Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) Julai, 2012 ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa BMC, Dk. Abel Makubi, wamekwishalipa mkopo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles