24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 6, 2022

WABUNGE WAIBANA SERIKALI STEMPU ZA KIELEKTRONIKI

Na GABRIEL MUSHI

Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeitaka Serikali kufanya tathmini ya kina kabla ya kuanza kutumia mfumo mpya wa stempu za kodi za kieletroniki (ETS) ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wamiliki wa viwanda nchini.

Mfumo huo wa ETS unalenga kudhibiti udanganyifu wa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa.

Kauli hiyo imetolewa jana Agosti 14, 2018 na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo iliyotembelea Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambapo pamoja na mambo mengine ilipokea malalamiko kuhusu mfumo huo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Innocent Bashungwa aliitaka Serikali kukaa na wamiliki wa viwanda nchini ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika mfumo huo ambao unadaiwa kukwamisha baadhi ya wawekezaji nchini kufungua viwanda vipya.

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mbunge wa Tabora Kaskazini, Musa Ntimizi (CCM) ambaye alisema licha ya serikali kuamua kujiandaa kutumia mfumo huo, bado zipo mbinu mbalimbali za kuwabana wazalishaji ambao ni wadanganyifu.

Wakati Mbunge wa Bahi Omary Badweli (CCM)ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo aliitaka serikali kutatua changamoto hizo haraka ikiwa ni pamoja na kuwapatia hati za ardhi wamiliki wa viwanda wenye nia ya kuwekeza Dodoma ili kuwavutia wawekezaji jijini humo.

Awali akiwasilisha mada kuhusu utendaji wa kampuni hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Robert Jarrin, Davis Deogratius alisema TBL haipingi matumizi ya mfumo huo wa ETS.

“Sisi hatupingi mfumo huu, ila tunaiomba serikali isiutumie mfumo huu kwenye bidhaa za bia, bali uitumie kwenye bidhaa za vinywaji vikali kwa sababu ni kweli kuna wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wanazalisha vinywaji vikali bila kulipa kodi wala kuzingatia sheria zozote na kuziingiza sokoni.

“Ila kwa upande wa uzalishaji wa bia ni vigumu kuwapo kwa udanganyifu kwani kila kitu kipo kiteknolojia, hadi chupa zimeandikwa tarehe, lakini pia tupo tayari kusaidiana na serikali kubuni mfumo sahihi ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hizi nchini,” alisema.

Alisema iwapo mfumo huo ukitumika katika uzalishaji wa bia, TBL italazimika kuilipa  Sh bilioni 27.6 kampuni ambayo imepewa zabuni ya kufunga mitambo ya kufunga stempu hizo, fedha ambazo haziendi serikalini.

“Sh bilioni 27.6 anapewa huyu mtu wa katikati, hapewi TRA, hiyo ni mbali na ushuru wenyewe, hii ina maana gharama za uzalishaji TBL zitaongezeka kwa zaidi ya asilimia 13. Hivyo wawekezaji wetu wanaweza kusita kutekeleza mpango wa kujenga kiwanda kingine kikubwa Afrika Mashariki kule Dodoma,” alisema.

Alisema TBL ina mpango wa kuwekeza Dola za Marekani milioni 100 (Sh bilioni 228.2), kujenga kiwanda kikubwa kuliko vyote nchini chenye uwezo wa kuajiri watu zaidi ya 700 na kitakachokuwa makao makuu wa TBL nchini.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, alisema Serikali ipo tayari kuanza mazungumzo na wadau hao wa viwanda nchini ili kuona namna bora ya kutekeleza mfumo huo wa ETS.

“Haya mambo yanazungumzika, utekelezaji utafanyika lakini tutakuwa tunaangalia, hayo si mambo ya kukata tamaa. Kwa sababu kulikuwa kuna wajanja wachache. Ndio maana serikali ikafikia maamuzi hayo,” alisema.

Mfumo huo wa ETS unatarajiwa kutekelezwa na kampuni Kampuni ya SCIPA kutoka Uswiss ambayo imeshinda zabuni hiyo nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,859FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles