WASHINGTON, MAREKANI
WAWAKILISHI wa Chama cha Democratic nchini Marekani wamefanya mgomo wa kukaa sakafuni na kugoma kuondoka bungeni kushinikiza upigaji kura ya kuidhinisha sheria kali ya udhibiti wa bunduki.
Zaidi ya wabunge 200 waliungana katika hatua hiyo ya kukaa sakafuni wakilitaka Bunge kupiga kura ya kuutanua uchunguzi wa historia ya mnunuzi na kuzuia ununuzi wa bunduki kwa watu, ambao wako kwenye orodha fulani za uchunguzi wa serikali.
Mgomo huo ulililazimu bunge hilo lenye wabunge wengi wa Republican kwenda mapumzikoni.
Sheria ya bunduki imetawala ajenda ya siasa za Marekani katika mwaka huu wa uchaguzi baada ya mtu mwenye silaha aliyedai kuwa mfuasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) kuishambulia klabu ya usiku ya mashoga mjini Orlando na kuwaua watu 49.
Hatua hiyo pia inakuja baada ya Baraza la Seneti nchini Marekani Jumatatu wiki hii kushindwa kupitisha vipengele vinne vya sheria ya udhibiti wa bunduki.