Na JUDITH NYANGE – MWANZA
MBUNGE wa Magu, Boniventura Kiswaga, amesema Mkoa wa Mwanza unanyemelewa na njaa kali kutokana na upungufu wa chakula uliopo nchini uliosababishwa na ukame na kuchangia kupanda kwa bei za vyakula.
Akizungumza juzi wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Kiswaga, alisema baadhi ya gharama za vyakula mkoani Mwanza ikiwemo mahindi zimeanza kupanda kwa kasi na sasa gunia moja la mahindi linauzwa kati ya Sh 95,000 hadi 100,000.
“Kupanda kwa bei ya vyakula kunaashiria huko tuendako hali itakuwa mbaya zaidi, wananchi wa Mwanza watakumbwa na njaa kwa kushindwa kumudu gharama za kujinunulia chakula.
“Nakishauri kikao hiki cha RCC kupitisha azimio la kuiomba Serikali ituletee chakula kutoka katika Ghala la Taifa la Hifadhi ya Chakula (NFRA), kitakachouzwa kwa wafanyabiashara kupunguza mfumuko wa bei ulioanza kujitokeza,” alisema Kiswaga.
Kiswaga ameshauri pia shule za Mkoa wa Mwanza zitakapofunguliwa Januari 2017 wanafunzi wasome mpaka saa nane mchana waruhusiwe kutoka kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kurudi nyumbani kwenda kula na kurejea shuleni kwani watakutana na maji tu na hawataweza kusoma wakiwa na njaa.
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, alisema suala la njaa kwa sasa si la mtu binafsi kutokana na hali iliyopo sasa inaashiria uwepo kwa upungufu mkubwa hivyo kukiomba kikao hicho kipitishe azimio la kuiomba Serikali kuleta chakula kitakachouzwa kupunguza mfumuko wa bei.
Alisema ingawa Rais Dk. John Magufuli alipokuwa katika ziara yake Sengerema alitoa tahadhari kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa mkoa utakaokumbwa na njaa mwaka huu, lakini suala hilo si la kisiasa bali ni uhalisia wa hali iliyopo ambayo imetokana na mvua kupungua sana msimu huu licha ya wakulima wengi kulima.
“Tunaiomba Serikali iridhie kwa kuwaruhusu baadhi ya wafanyabiashara walete chakula kutoka ghala la Serikali kupitia utaratibu uliopo kitakachouzwa mkoani Mwanza,” alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Sumve, Richard Ndasa, alisema jamii ya Wasukuma hawana kawaida ya kuomba chakula serikalini lakini kutokana na mabadiliko ya hali na mvua kupungua imewalazimu kufanya hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema ni vyema wakuu wa wilaya wakaziagiza kamati za maafa za wilaya wakafanye tathmini.