NA KULWA MZEE-DODOMA
BUNGE limewafunga mdomo wabunge ambao wamekuwa wakitumia mjadala wa Ripoti ya Pili ya Makinikia, kutaka marais wastaafu wafutiwe kinga ili washtakiwe kwa kuliingizia taifa hasara ya matrilioni ya shilingi, kwa kusema jambo hilo ni kinyume na katiba.
Wakati Bunge likifikia uamuzi huo kutokana na mwongozo uliotolewa jana asubuhi na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan Zungu, Rais Dk. John Magufuli naye amevionya vyombo vya habari kuwahusisha na ripoti hiyo marais wastaafu, Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, katika taarifa yake jana, alisema vyombo vya habari vina dalili ya kupotosha kampeni ya kujikomboa kiuchumi iliyopo sasa.
Wabunge
Hoja ya kutaka marais wastaafu wasiendelee kujadiliwa kwenye suala hilo, ilianzishwa na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, alipoomba mwongozo wa kiti juu ya suala hilo.
“Kwenye hotuba ya bajeti umekuwapo mjadala kuhusiana na mapato yanayopatikana kupitia kwenye vyanzo mbalimbali, yakiwamo madini.
“Wakati wabunge wanaendelea kuchangia na kutafakari kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli na hasa baada ya kuunda kamati mbili ambazo zilitoa picha kuhusiana na rasilimali hizi katika nchi, yamejitokeza mambo ambayo nimelazimika kuomba mwongozo.
“Ibara ya 66 na vifungu vidogo katika ibara hiyo, inazungumzia kinga ya madaraka ya rais, lakini katika mjadala huu kumejitokeza baadhi ya wabunge wakiunganisha mjadala huu na kuwaingiza marais wastaafu na kutaka wachukuliwe hatua kama vile wana hatia, lakini kwa kupitia kazi nzuri ya Rais Magufuli.
“Je, Bunge hili lipo sahihi? Naomba sana mwongozo wako mheshimiwa mwenyekiti ili suala la bajeti na kazi nzuri iliyofanywa na rais viweze kutenganishwa,” alisema.
Lissu
Kabla ya Zungu kujibu mwongozo huo, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alinyanyuka na kusema: “Masuala yaliyozungumzwa ya marais wastaafu ni sahihi kwa sababu Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ndiye aliyesaini leseni ya Bulyanhulu, Nzega na Geita akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, hakuwa na kinga kipindi hicho wala hana kinga leo.
“Kikwete ana kinga kwa yale mambo ambayo aliyafanya kama rais, hivyo hoja ya kutaka wawekewe ulinzi wasiokuwa nao naomba mwenyekiti usikubalianae nayo.”
Zungu
Akitoa uamuzi wa kiti, Zungu alisema viongozi wastaafu walitumia nguvu na uwezo wa kutumikia nchi, hivyo hawapaswi kushambuliwa kwa mujibu wa Katiba.
Aliwataka wabunge kujielekeza katika mjadala uliopo bungeni kwa sasa bila kutumia fursa hiyo kuwashambulia viongozi wastaafu.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 46.3, inatoa kinga kwa rais aliyekuwapo madarakani na kwa rais mstaafu.
“Ibara hii inaelekeza kwamba itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai, au la kumdai mtu ambaye alikuwa anashika madaraka ya rais, baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilolifanya wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya rais.
“Kwa mujibu wa Katiba, isipokuwa tu kama aliacha urais baada ya Bunge kupitisha azimio kwa mujibu wa ibara ya 16 a,” alisema.
Zungu alisema kanuni ya 64 inatoa makatazo kwa masuala mbalimbali ambayo hayaruhusiwi wakati wa mjadala bungeni.
Alisema kanuni hiyo pamoja na mambo mengine, inazuia kujadili mwenendo na utendaji kazi wa rais aliyeko madakarani na kanuni hiyo inazuia pia kuzungumza mwenendo wa marais wastaafu, ikiwa rais mstaafu huyo alitumika nchi kwa miaka yote iliyotakiwa katika katiba na kuondoka madarakani bila kuondolewa na Bunge au kwa namna yeyote ile.
Kibano vyombo vya habari
Wakati huohuo, taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilimnukuu Rais Magufuli akisema: “Nimesoma ripoti zote mbili, hakuna mahali ambako mzee Mkapa na mzee Kikwete wametajwa.
“Vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia taifa, viwaache wapumzike.”
Dk. Mwakyembe
Naye Dk. Mwakyembe katika taarifa yake alisema baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii, vimetumia jambo hilo kurusha kila aina ya tuhuma dhidi ya marais wastaafu Kikwete na Mkapa bila kujali madhara ya siasa na jamii na kwa uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola.
“Kutokana na msingi huo, naviasa vyombo vya habari nchini na mitandao ya jamii kuacha mara moja mwelekeo huo hasi, ambao una kila dalili ya kututoa kwenye mstari na kupotosha kampeni tuliyonayo ya kujikomboa katika uchumi,” alisema.
Azimio la kumpongeza JPM
Katika hatua nyingine, Bunge limeazimia kumpongeza Rais Magufuli kwa juhudi, uthubutu na uzalendo wa hali ya juu wa kufungua njia itakayowezesha taifa na wananchi kwa ujumla kufaidika na rasilimali za nchi.
Azimio hilo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Haki, Maadili na Madaraka, Kapteni George Mkuchika (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Newala Mjini.
Mkuchika alisema Bunge lipo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa kadiri itakavyohitajika katika kuhakikisha juhudi, uthubutu na uzalendo aliouonyesha haupotei bure bali unakuwa chachu ya kuhakikisha sekta ya madini inachangia katika kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.