23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WA TANZANIA, KENYA WAVAMIWA AFRIKA KUSINI

Gitobu Imanyara
JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

WABUNGE wa Bunge la Afrika (PAP) kutoka Tanzania, Kenya na Msumbiji wamevamiwa na majambazi walipokuwa wakitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo mjini hapa wakienda hotelini.

Mmoja ya wabunge hao kutoka Kenya alipigwa   na majambazi hao alipokuwa akijaribu kuzozana nao wasiwaibie.

Imeelezwa kuwa majambazi hao walikuwapo uwanjani hapo Jumapili wabunge hao walipowasili na kuwafuatilia kwa gari wakati wakielekea Hoteli ya Mercure.

Walipofika hotelini hapo, waliwazingira na kuwapora fedha, hati za kusafiria na mikoba kwa mtutu wa bunduki.

Mkalimani wa wabunge wa Kenya pia alijeruhiwa wakati majambazi hao walipompiga kwenye paji la uso kwa kitako cha bastola.

Ingawa wabunge waliokuwa kwenye msafara huo hawakutajwa, lakini Tanzania inawakilishwa katika Bunge hilo la Afrika na Dk. Gertrude Mongella, Omar Sheha Mussa, Athumani Janguo, Prof. Feethan Banyikwa na John Cheyo.

Wabunge kutoka Kenya ni Gitobu Imanyara, Musa Sirma, Rachel Shebesh, Ali Bahari na Gideon Mungaru huku wanaoiwakilisha Msumbiji ni Macamo Nataniel, Dique Angelina, Munhawa Salvador, José Manteigas na Eduardo Mulémbwè.

Mlolongo huo wa mashambulio dhidi ya wabunge walioanza kikao chao Jumatatu, uliwafanya waje juu siku hiyo wakimtaka Spika asimamishe shughuli za Bunge hadi suala la usalama wao litakapotatuliwa.

“Kikao cha Bunge kiliendelea baada ya kuhakikishiwa na polisi na Serikali ya Afrika Kusini kuwa vitendo hivyo havitatokea tena,” alisema Rais wa PAP, Roger Nkodo na kuongeza kuwa suala la usalama ni wajibu wa nchi mwenyeji, si Spika wa Bunge.

Agosti mwaka jana, wabunge kutoka Uganda walishambuliwa na watu wenye silaha wakati wakiingia katika nyumba ya wageni ya KariBou-Inn katika kitongoji cha Johannesburg na kupoteza hati za kusafiria na vitu vyao binafsi.

Mwezi mmoja kabla, Mbunge Aissatou Sow Diawara kutoka Senegal, alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati akiondoka uwanja wa ndege wa Johannesburg, huku wenzake watatu kutoka Namibia wakiporwa mizigo yao.

Mashambulio mengine dhidi ya wabunge wa PAP yaliripotiwa Machi na Julai mwaka jana na Agosti na Oktoba mwaka juzi.

Kutokana na mashambulio hayo ya mara kwa mara, wabunge wengi wameonyesha kukerwa na kusema wakati umefika kwa Bunge hilo la Afrika kuhamishwa kutoka Afrika Kusini kwa sababu hakuna usalama wa kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles