27.8 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Wabunge: Ndoa za utotoni ni janga kubwa

Gabriel Mushi, Dar es Salaam 

‘Sifa ni binti mwenye umri wa miaka 14 aliyetoka katika familia masikini. Licha ya kuwa na ndoto za kuwa mwalimu, wazazi wake walimuoza baada ya kupokea mahari ya ng’ombe na mbuzi.

Hata hivyo, binti huyo alipoteza maisha baada ya kujifungua na kupata fistula kutokana na via vyake vya uzazi kuwa vidogo, huku mtoto aliyejifungua naye akifariki dunia baada ya kukaa muda mrefu ndani ya mfuko wa uzazi’.

Kisa hicho cha Sifa ni moja kati ya vingine tofauti vinavyowapata watoto wa kike wa Tanzania ambao takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa asilimia 36 ya watoto wa kike huolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Sifa na wasichana kama yeye ni waathirika wa sheria ya Sheria ya ndoa ya 1971 (LMA, 1971) ) ambayo kimsingi inaruhusu wasichana wadogo wa miaka 15 kuolewa. Kwa wavulana umri huwekwa miaka 18.

Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsi, Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) hivi karibuni umekutana na wabunge mbalimbali ili kujadilia na kuhamasisha njia sahihi za kubadilisha sheria hizo hizo zinazokiuka haki za binadamu.

TECMN ni muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 50 yanayoshirikiana kukomesha ndoa za utotoni nchini ikiwamo Shirika la Utu wa Mtoto(CDF, Kituo cha Haki za Kisheria na za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Wanawake wa Tanzania (TAWLA).

Mwenyekiti wa TECMN, Valeria Msoka anasema miongoni mwa masuala yanayoathiri ustawi wa mtoto wa kike ni lile la ndoa za utotoni, licha ya jitihada za miaka kadhaa ya kuziondoa.

“Kitaifa, wasichana wawili kati ya 5 wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18. Na ingawa ndoa za utotoni hufanyika takribani nchi nzima, mikoa mitano inayoongoza ni Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora kwa asilimia 58, mara kwa asilimia 55, Dodoma na 51 na Lindi kwa asilimia 48. Mkoa kiwango cha chini kabisa ni Iringa kwa 8%. Lakini, Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) unasema idadi inayokubalika ni sifuri,” anasema.

Anasema katika kujenga ushawishi mabadiliko ya sera ili kutokomeza ndoa za utotoni, mtandao huo ulikutana na wabunge hao pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali Novemba mweaka huu jijini Dodoma.

“Kutokana na ufadhili wa mashirika kama vile UNFPA, Amplify Change, PLAN International, Balozi za Canada na Ufaransa na Foundation for Civil Society, TECMN ilionyesha madhara ya ndoa za utotoni kwa mtoto wa kike ambaye mwili wake haujaumbika kikamilifu ambayo ni pamoja na vifo vya wasichana hao, watoto wachanga na uwezekano mkubwa wa maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na VVU/UKIMWI,” anasema.

Aidha, Msoka anasema ukosefu wa elimu unasababisha pia ukosefu wa ujuzi na huibua uhaba wa ajira na hivyo kuleta utegemezi katika ndoa ambao unamfanya msichana asiweze kuondoka hata kama mume wake anamnyanyasa kwa vile anamtegemea kimaisha.

Mratibu wa Mtandao huo, Michael Sungusia anasema kuwa kunahitaji ushirikiano kati ya wadau mbalimbali na wabunge ili kutokomeza sheria hizo kandamizi.

“Hitaji la kuwa na watetezi na washawishi ndani ya Bunge ni kwa sababu wabunge wana nafasi ya kipekee ya kuendeleza hoja hii na kuiwekea mifumo ya utekelezaji ndani ya nchi na hata nje.

“Wanaweza kuongoza uundaji wa sheria na sera husika, kupitisha bajeti, kufuatilia utekelezaji na na kuhakikisha uwajibikaji katika mikataba ya kitaifa na kimataifa. Wanaweza kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika, ikiwa ni pamoja na zile za mtoto wa kike, ili kuhamasiha utashi wa kisiasa na nia ya kutokomeza nda za utotoni” anasema.

Anasisitiza kuwa Wabunge kuhusu jukumu lao kama watunga sheria na kwamba wajibu wao katika kukomesha ndoa za utotoni umejikita katika marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Hoja hiyo pia inaungwa mkono na Mwanasheria Gertrude Dyabene, kutoka LHRC, ambaye anataja baadhi ya sheria ambazo zinakinzana na sheria ya ndoa na ambazo zilipitishwa na Bunge ili kumlinda mtoto wa kike.

“Hizi ni pamoja na Kanuni za Adhabu, Sehemu 130 (2) (e) na 138, ambazo zinasema kuwa mtu anayefanya ngono kwa ridhaa au bila ridhaa na msichana chini ya miaka 18 anakuwa amebaka. Sheria ya ndoa inaruhusu msichana mwenye umri wa miaka 14 aolewe kwa ridhaa ya mahakama na kwamba ndoa imekamilika tendo la ndoa likifanyika. Chini ya Kanuni za Adhabu, ukamilifu huo ni kosa na hivyo kustahili adhabu.

“Sheria ya Elimu, Marekebisho ya  2016, ambayo inasema ni kinyume cha sheria kuwa na mahusiano ya kingono au kumpa mimba msichana mwanafunzi. Wasichana hawa wa shule wanalazimishwa  kuolewa kwa sababu sheria ya ndoa inaruhusu.

“Pia Sheria ya Mkataba ambayo inasema umri wa mkataba kuwa ni miaka 18 kwa imani kwamba katika umri kama huo mtu anaweza kufahamu matokeo ya matendo yake. Kwamba ndoa ni aina ya mkataba lakini mtoto wa kike ananyimwa haki yake wakati wazazi au mahakama inakubali kwa niaba yake. Hii huvunja haki yake ya mkataba kuhusiana na ndoa yake mwenyewe,” anasema.

Naye Wakili Barnabas Kaniki, wa Chama cha Wanasheria wa Wanawake wa Tanzania (TAWLA) anasema; “Sheria ya mfano ni zana muhimu sana kwa Tanzania tunapofakari kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

“Nchi jirani ya Malawi, ambayo ni sehemu ya SADC, mwezi Februari 2017 ilibadilisha katiba yao ili kuzuia ndoa za utotoni kwa kuweka umri wa ndoa kuwa 18 kwa Wavulana na Wasichana,” anasema.

Wabunge walonga

Baadhi ya wabunge walioshiriki mkutano huo walionesha nia ya dhati kubadilisha sheria hizo.

Mbunge wa viti maalumu, Martha Mlata (CCM) anasema; “inahitajika kutangazwa kuwa ndoa za utotoni ni janga la kitaifa ili kama taifa tunachukua hatua dhidi ya utamaduni wenye madhara na ambao umepitwa na wakati”.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ileje, Janet Mbene anasema  “inasikitisha kwamba wakati serikali inapozungumzia kuendeleza wananchi wake kuna kundi fulani ndani ya wananchi wake hao ambalo linanyimwa hayo maendeleo. Suala lingine linalonisumbua ni kwamba sheria nyingi zinazoathiri na wanawake na watoto ndio ambazo zimekwama, miaka nenda miaka rudi…. lakini miswaada mingine inapitishwa kwa dharura.”

Naye Mbunge Malindi, Ali Saleh (CUF), “Utamaduni na Dini havipaswi kuwa sababu ya kumyima mtoto wa kike haki zake za msingi. Kwa hiyo tunapaswa kuacha tofauti zetu za dini na za chama na tunahitaji kudai hii haki kwa kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971.”

Spika wa Bunge, Job Ndungai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi wote walilitambua tatizo na haja ya kukomesha ndoa za utotoni.

Spika Ndugai anasema”tunapaswa kuwaelimisha wananchi pamoja na viongozi wa dini na jadi kwani hili ni jambo nyeti na linagusa hisia. Ikiwa tunawaelimisha na wanaelewa basi bunge litakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kulizungumzia vizuri.”

Naye Dk. Kilangi  anasema ingawa suala hili ni nyeti, halimaanishi kuwa haliwezi kupatiwa suluhisho.

“kwa bahati mbaya sheria ya ndoa ina masuala mengi ambayo inafanya kubadilishwa kwake kuwa jambo la hisia na vurugu; ni sheria inayogusa jadi, dini na sheria za India ambazo tulizichukua. Endeleeni kushawishi na hatimaye itatokeka, lakini pia ieleweke kuwa sheria huchukua muda kubadilishwa, kama vile Roma haikujengwa kwa siku moja. ” anasema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles