24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE, MAWAZIRI WAKACHA MKUTANO WA BUNGE

Na Fredy Azzah-Dodoma


MKUTANO wa 11 wa Bunge  ulianza  Dodoma jana huku ukihudhuriwa na idadi ndogo ya wabunge na mawaziri.

Mkutano huo wa Bunge la Bajeti   leo unatarajiwa kuanza kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

Jana ulianza kwa kuwaapisha wabunge wa CCM, Dk Godwin Mollel (Siha) na Maulid Mtulia (Kinondoni).

Kutokana na mahudhurio ya watungasheria hao kutokuwa mazuri, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM),  alisimama na kuomba mwongozo wa Naibu Spika kwa kuhoji  endapo kiapo cha wabunge hao wapya kilikuwai halali ama laa.

Ikumbukwe kuwa awali Dk. Mollel alikuwa Mbunge wa    Siha  kwa tiketi ya Chadema huku Mtulia pia akiwa Mbunge wa Kinondoni  kwa tiketi ya CUF kabla ya kujiuzulu ubunge na kujiunga na CCM.

Jana wakati wakila kiapo cha uaminifu mbele ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wabunge wa upinzani waliokuwamo bungeni walikuwa takriban wanne kutoka CUF.

Wabunge hao ni kati ya walioingia bungeni baada ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwavua uanachama wabunge wanane wa viti maalumu na nafasi zao kuteuliwa wabunge wengine   na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wabunge wa Chadema waliokuwamo ni Chacha Marwa na Serengeti na Joyce Sokombi wa viti maalum.

Hadi  kipindi cha maswali na majibu kinamalizika, wabunge wa upinzani walikuwa 18, huku   wa CCM wakiwa takribani nusu ya idadi yao.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu,  Mlinga  aliomba mwongozo kwa Spika  akihoji kama kiapo cha wabunge hao kilikuwa halali kwa sababu waliapa huku wabunge wakiwa wachache.

Alihoji pia endapo wabunge walioudhuria bunge hilo watalipwa posho kwa sababu ya akidi kutotimia na ni hatua gani zitachukuliwa kwa wale ambao hawakuhudhuria.

Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia alisema, “Mlinga kauliza kuhusu akidi, kwa sababu anasema kwa kanuni inatakiwa wabunge wawe nusu, lakini kanuni ya 77 (1-5), inasema kuhusu shughuli za uendeshaji wa Bunge na akidi.

“Akisema akidi haijatimia sijui yeye ndiye kahesabu hao wabunge ama vipi, niseme tu suala la akidi ni wakati wa kuanza kikao kwa hiyo mwongozo anaoutaka sasa haupo kikanuni, kwa hiyo walioapishwa wameapishwa  halali,” alisema Dk Tulia.

Idadi hiyo ndogo ya wabunge iliendelea kuwa hivyo mpaka Bunge linaahirishwa mchana ambako pia mawaziri na manaibu waziri waliokuwa wameketi kwenye viti vyao walikuwa chini ya 10.

Mbunge na wimbo wa Taifa

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM),  aliomba mwongozo wa Spika akisema wimbo wa Taifa ulioimbwa wakati wa kufungua mkutano huo wa 11 siyo wimbo rasmi wa Taifa.

Alisema wimbo huo una makosa mengi kuanzia kwenye ala, mdundo na maneno.

Alisema wimbo wa taifa unaoimbwa Bungeni unatofautiana na ule unaoimbwa kwenye maeneo mengine   ikiwamo kwenye shughuli muhimu.

Mbunge huyo  alisisitiza wimbo huo haukuwa ule uliothibitishwa na mamlaka husika.

Dk. Tulia, akijibu mwongozo huo alisema anahitaji muda akasikilize tena wimbo huo   abaini tofauti hizo alizoziainisha mbunge huyo.

Alshabaab na mkaa wa Tanzania

Wakati huohuo, Waziri wa Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema kiasi kikubwa cha mkaa unaotoka nchini unaenda kutumiwa kwenye mataifa mengine ikiwa ni pamoja na Somalia na Uarabuni.

Alikuwa akihitimisha hoja wakati wa kupitisha Azimio la Bunge la kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Makamba alisema mkaa huyo hutolewa nchini kupitia bandari za Bagamoyo, Mbweni na nyingine za Pwani kwenda Pemba na baadaye Shimoni Mombasa.

“Ukiangalia mkaa mwingi unaoenda Pemba ni  ambao hauendani na watu wa Pemba, ukifika Pemba wanapeleka Shimoni na baadaye Somalia, unaenda kuwa mtaji kwa Alshabaab.

“Mwingine unaenda uarabuni kuchoma kondoo kwa sababu waarabu wanapenda mkaa mzuri wa kuchoma kondoo.

“Kwa hiyo utaona mkaa unakatwa huku unaenda kunufaisha watu wengine huko,” alisema Makamba.

Awali, wakichangia azimio hilo, Mbunge wa Nkenge, Balozi Diodorus Kamala (CCM), alisema nchi kuridhia makubaliano hayo kuna manufaa mengi ikiwa ni pamoja na kufaidika na Sh trilioni 195 zitakazotolewa kwa nchi zilizouridhia   ziweze kuutekeleza.

“Hizi fedha ni kama dola za Marekani bilioni 70, na zitakagawanywa kwa takriban  nchi 70 tu, kwa hiyo kuridhia huu mkataba kuna faida nyingi,” alisema Kamala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles